Serikali yaitaka TASAC kuandaa wataalamu zaidi

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

SERIKALI imeitaka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), kuandaa wataalamu wa kutosha wa sekta ya bahari ili kuendana na kasi ya ukuaji wa biashara katika bandari za Tanzania ikieleza kuwa mahitaji ya manahodha, wasaidizi wa mabaharia na wataalamu wengine yataendelea kuongezeka.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema ukuaji mkubwa wa biashara katika bandari unaonesha mahitaji ya wataalamu wa sekta ya bahari yanaongezeka kwa kasi.

Aidha, amefafanua kuwa kiwango cha mizigo kilichokuwa kinatarajiwa kufikiwa mwaka 2030 kilifikiwa mapema mwaka 2022 kutokana na uongozi madhubuti, kuimarika kwa diplomasia ya uchumi na ushiriki wa sekta binafsi.

2-15 Serikali yaitaka TASAC kuandaa wataalamu zaidi

Kihenzile amesema ongezeko hilo la mizigo linamaanisha kuwa kutahitajika manahodha, wasaidizi wa mabaharia na wataalamu wengine wengi zaidi ili kuhudumia shughuli zinazopanuka katika sekta ya usafiri wa majini.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka TASAC kutotekeleza jukumu la udhibiti pekee, bali kushirikiana na Serikali kuweka mikakati ya kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaokidhi mahitaji ya sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Wakati huo huo, Kihenzile amesema Serikali itaendelea kulinda uwekezaji wa vyombo vya majini pamoja na mali za wawekezaji ili kuweka mazingira salama ya biashara.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wawekezaji wanaowekeza katika meli, boti na vyombo vingine vya majini wanaendelea kufanya shughuli zao bila hofu, huku ulinzi wa raia, wasiokuwa raia na mali zao ukipewa kipaumbele kupitia taasisi husika za Serikali.

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza imani ya wawekezaji na kuvutia uwekezaji zaidi katika uchumi wa buluu, ambao unaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na ajira kwa Watanzania.

3-14 Serikali yaitaka TASAC kuandaa wataalamu zaidi

Pia amewapongeza watumishi wa TASAC kwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi, akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo ili kuhakikisha manufaa ya sekta ya bahari yanawanufaisha Watanzania wote na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *