Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inatarajia kuanzisha shirika la ndege litakaloongeza ushindani, kupunguza gharama za nauli na kurahisisha usafiri kati ya Zanzibar na Arusha, hatua itakayochochea utalii, biashara na uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 17 Novemba 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Madiwani wa Jiji la Arusha wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kuvutia uwekezaji na kuandaa vifurushi vya pamoja vya utalii kati ya Zanzibar na Arusha.
Aidha, ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kushirikiana kutangaza vivutio vya maeneo hayo katika maonesho ya kimataifa, huku akieleza kuwa Zanzibar inaendelea kupokea zaidi ya watalii laki moja kwa mwezi na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake, Waziri Paul Makonda amesema ziara ya viongozi wa Mkoa wa Arusha Zanzibar inalenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya utalii, pamoja na kuboresha huduma kwa wageni wanaotembelea maeneo mbalimbali nchini.
Amesema hatua hiyo inaunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza idadi ya watalii na manufaa ya kiuchumi yatokanayo na sekta hiyo.

Amesema hatua hiyo inaunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza idadi ya watalii na manufaa yatokanayo na sekta hiyo.