EWURA yatoa somo kupunguza bili kubwa za maji, umeme

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA CCC), imewataka wananchi kufuata kanuni sahihi za matumizi ya nishati na maji, ikisema hatua hiyo itasaidia kupunguza bili kubwa, kuongeza usalama na kulinda haki za watumiaji.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji Mwandamizi wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, amesema mamlaka hiyo imefika katikati maonesho hayo kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za umeme, mafuta, gesi asilia pamoja na maji safi na usafi wa mazingira ili waweze kufanya maamuzi sahihi wanapotumia huduma hizo.

“EWURA imeanzishwa kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji. Tumefika hapa kuhakikisha mtumiaji anapata taarifa sahihi, kwa sababu tunaamini mtumiaji mwenye taarifa sahihi ndiye mwenye uwezo wa kuelewa haki zake na wajibu wake wa msingi,” amesema Lugiko.

Amesema kwa upande wa umeme, watumiaji wanapaswa kutumia mafundi wenye leseni ya EWURA wakati wa kufunga miundombinu ya umeme na kuhakikisha wanatumia vifaa bora ili kuepuka matumizi makubwa ya umeme na ajali.

“Ni lazima utumie mafundi wenye vibali na leseni za EWURA. Pia tumia vifaa bora kwa sababu vifaa vibovu vinaweza kusababisha matumizi makubwa ya umeme na hata kuunguza vifaa vyako,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi kukagua miundombinu ya umeme majumbani kila baada ya miaka mitano, akieleza kuwa wakati mwingine umeme unaonekana kuisha haraka kutokana na hitilafu za miundombinu.

1-18 EWURA yatoa somo kupunguza bili kubwa za maji, umeme

Kuhusu huduma za maji, Lugiko amesema kabla ya kulalamikia bili kubwa, watumiaji wanapaswa kuhakiki usomaji wa mita na kuchunguza kama kuna uvujaji wa maji katika maeneo yao.

“Kabla haujakimbilia kusema bili ni kubwa, jiridhishe kama usomaji wa mita uko sahihi. Pia chunguza kama kuna mivujo yoyote ya maji katika eneo lako, kwa sababu inaweza kuwa chanzo cha bili kubwa,” amesema.

Kwa upande wa matumizi ya gesi ya kupikia, amewataka wananchi kusafirisha mitungi ikiwa imesimama na kuiweka sehemu yenye hewa ya kutosha ili kupunguza hatari za milipuko endapo kutatokea uvujaji.

Lugiko pia amewataka watumiaji wa mafuta kuhakikisha wanafahamu bei zinazotangazwa na EWURA kila Jumatano ya kwanza ya mwezi, kuhakiki pampu inaanza kwenye sifuri wakati wa kujaza mafuta na kuchukua risiti kila wanaponunua mafuta.

“Hakikisha pump inaanzia kwenye sifuri ili upate ujazo halisi wa mafuta. Muhimu zaidi chukua risiti kwa sababu ndiyo ushahidi wako endapo kutatokea changamoto,” amesema.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka kununua mafuta katika vituo visivyo na leseni, huku akibainisha kuwa malalamiko mengi yanayowasilishwa EWURA yanahusu huduma za maji na umeme kwa sababu ni huduma zinazogusa maisha ya kila siku.

Aidha Lugiko amewahamasisha Watanzania kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisema matumizi ya umeme na gesi ni salama, yanaokoa muda na ni rafiki kwa mazingira.

“Tunawasisitiza watumiaji wasiogope kutumia umeme kwa sababu ni nishati salama, inaokoa muda na pia inapunguza uharibifu wa mazingira,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *