FCC yawajengea uwezo wajasiliamali kushindana kibiashara Sabasaba

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

TUME ya Ushindani (FCC) imesema imeweka mkazo katika kuwajengea uwezo wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu ushindani wa haki, ulinzi wa mlaji na namna ya kukabiliana na bidhaa bandia kupitia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi na wafanyabiashara kwa kuwapatia elimu itakayowasaidia kukuza biashara zao katika mazingira ya ushindani wa haki.

Amesema pamoja na kutoa elimu, FCC imepeleka huduma zake karibu na wananchi kwa kupokea na kushughulikia malalamiko papo kwa papo, kusajili mikataba pamoja na kutoa huduma mbalimbali zinazotolewa na tume hiyo.

2-16-1024x682 FCC yawajengea uwezo wajasiliamali kushindana kibiashara Sabasaba

Feruzi amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo, FCC imewafikia zaidi ya wajasiriamali 700 kupitia semina na ziara katika mabanda mbalimbali, ambapo wameelimishwa kuhusu ushindani wa haki, ubunifu wa biashara na fursa zinazotolewa na Serikali kwa sekta binafsi.

Ameeleza kuwa sehemu ya walengwa wakuu ni vijana wabunifu (startups), ambao wamehamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na FCC kwa kufika katika ofisi zake za kanda zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya ili kupata ushauri na mwongozo wa kukuza biashara zao.

Kwa mujibu wa Feruzi, utoaji wa elimu hiyo utaendelea hata baada ya maonesho ya Sabasaba kumalizika, ambapo FCC imejipanga kuwafikia makundi mbalimbali ya wafanyabiashara nchini ili kuendelea kujenga mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki na uchumi shindani.

Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika maonesho hayo ili kupata huduma na elimu inayotolewa na FCC pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuimarisha biashara na kulinda maslahi ya walaji nchini.

3-15-1024x682 FCC yawajengea uwezo wajasiliamali kushindana kibiashara Sabasaba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *