Dkt. Samia kufungua mkutano wa Kimataifa wa madini(TMIC 2026)

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), utakaofanyika Novemba 19 hadi 21 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Mkutano huo unatarajiwa kukutanisha washiriki 1,715 waliothibitisha kushiriki kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo washiriki 226 kutoka mataifa mbalimbali duniani, mawaziri wa madini kutoka nchi mbalimbali, viongozi wa kampuni za kimataifa, taasisi za fedha, wawekezaji na wadau wengine wa sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 17, 2026 kuelekea mkutano huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi, unalenga kuhamasisha matumizi ya rasilimali za madini katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kuhakikisha madini yanaongezwa thamani nchini kwa manufaa ya Taifa.

Mavunde amesema mkutano huo utakuwa jukwaa la kuvutia uwekezaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia na utaalamu, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kutangaza utajiri wa Tanzania na kutafuta masoko ya madini nje ya nchi.

Pia utatoa fursa kwa washiriki kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu maendeleo ya sekta hiyo.

Amesema kutakuwa na watoa mada zaidi ya 57 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na Marekani, watakaowasilisha mada zinazohusu masuala mbalimbali ya sekta ya madini, hususan uongezaji thamani wa rasilimali hizo.

Ameeleza kuwa mafanikio ya sekta hiyo yameendelea kuonekana, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa uliongezeka hadi asilimia 10.3 mwaka 2025 kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024, huku thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ikipanda kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi bilioni 5.40 mwaka 2025.

Aidha, amesema mapato ya Serikali yatokanayo na sekta ya madini yameongezeka kutoka Sh bilioni 526 mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh trilioni 1.39 mwaka wa fedha 2025/26.

Mkutano huo pia utaambatana na maonesho ya madini, mikutano ya kibiashara kati ya kampuni, mafunzo ya uongezaji thamani madini na Hafla ya Usiku wa Madini itakayohusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri.

Aidha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kufunga mkutano huo Novemba 21 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *