Na Benny Mwaipaja, Antalya-Uturuki
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imepanga kutumia mbinu mchanganyiko na mikakati minnne itakayosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ikiwemo sera za kikodi na kimiundombinu ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Balozi Omar amesema hayo mwishoni mwa juma jijini Antalya nchini Uturuki wakati akifanya majumuisho baada ya kushiriki mkutano wa Umoja wa Mtaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP31, uliowashirikisha viongozi wa mataifa mbalimbali na mashirika ya kimataifa.
Ametolea mfano wa uwekezaji katika reli ya kisasa ya SGR, ambayo inatajwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa tani 66 kila mwaka, pamoja na kuimarisha usafiri wa mabasi ya mwendo kasi yanayotumia gesi asilia (CNG) na kuangalia uwezekano wa kutumia mabasi ya umeme.
Katika eneo la pili, Balozi Omar amesema kuwa mageuzi ya mabadiliko ya tabianchi lazima yaendane na ajenda ya maendeleo ya viwanda endelevu, kulingana na Dira 2050.
Eneo la tatu linahusu ajira, hususan kwa vijana na wanawake ambapo alieleza kuwa Serikali inashirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kubadilisha ushoroba wa kati wa reli ya SGR kuwa eneo kubwa la kiuchumi litakalozalisha ajira endelevu kupitia uwekezaji binafsi.
Balozi Omar amesema kuwa changamoto kubwa iliyoibuliwa ni upatikanaji wa fedha, ambapo kuna nakisi ya dola bilioni 12 katika utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi na kwamba ili kuziba pengo hilo, serikali inahimiza ubia kati ya sekta ya umma, mashirika ya kimataifa, na sekta binafsi ili kufikia matokeo ya kunufaishana kwa pande zote.
Kuhusu mwelekeo wa kimataifa, alisema mjadala mkubwa wa mkutano huo uligusia pia suala la nishati safi ya kupikia na uchakataji wa madini muhimu ambapo ilibainika kuwa zaidi ya asilimia 82 ya uchakataji wa madini hayo hufanyika katika nchi chache zilizoendelea, hali inayoongeza utegemezi.
Amesema Tanzania imesisitiza msimamo wake wa kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi (beneficiation) ili kukuza viwanda vya ndani badala ya kuwa wasambazaji wa malighafi pekee.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akishiriki Mkutano wa Viongozi: Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na washiriki wengine kutoka sekta ya fedha, viwanda na taasisi za kimataifa ili kubadilisha malengo ya ukuaji wa viwanda wa kijani kuwa miradi inayoweza kuwekezwa, minyororo imara ya ugavi na ajira bora.Mkutano wa uchumi wa Kijani uliofanyika Kando ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi COP 31, uliofanyika Jijini Antalya ncjini Uturuki.