Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MCHANGO wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024 hadi asilimia 10.3 mwaka 2025, huku thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ikipanda hadi Dola za Marekani bilioni 5.4, hatua inayoonesha kuimarika kwa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Taifa.

Katika miezi minne ya mwaka wa Fedha 2026/2027 Sekta hiyo imekusanya Shilingi bilioni 604 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 583 sawa na asilimia 103 ya lengo.

IMG-20261117-WA17151-682x1024 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Mafanikio hayo yanakwenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuongeza thamani ya madini nchini badala ya kutegemea uchimbaji na uuzaji wa malighafi, ili kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali hizo.

Katika kuharakisha mkakati huo, Tanzania inatarajia kukutanisha zaidi ya wadau 1,700 wa ndani na nje ya nchi katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

1003782592-1024x683 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa hadi Novemba 17, washiriki 1,715 walikuwa wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo, wakiwamo 226 kutoka mataifa mbalimbali.

Amesema pia mawaziri wa madini kutoka Afghanistan, Kenya, Uganda, Mali, Rwanda, Burundi, Saudi Arabia na Somalia wanatarajiwa kushiriki pamoja na watoa mada zaidi ya 57 kutoka Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na Marekani.

1003782593-1024x683 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Mavunde amesema mkutano huo utakuwa fursa ya kuvutia uwekezaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia na utaalamu, kupanua masoko ya madini na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

Ameongeza kuwa washiriki watapata nafasi ya kujadili mipango ya Serikali na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi. Kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi.’

IMG-20261117-WA1717-1024x682 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo, amesema mapato ya Serikali yatokanayo na madini yameongezeka kutoka takribani Sh bilioni 526 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.39 mwaka wa fedha 2025/2026, huku thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ikipanda kutoka Dola bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi Dola bilioni 5.40 mwaka 2025.

Amesema ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo pia umeimarika, ambapo ajira rasmi zilifikia 19,874 hadi Aprili 2025, huku asilimia 97.4 zikiwa za Watanzania.

IMG-20261117-WA1714-1024x682 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Aidha, ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazawa umeongezeka kutoka Sh bilioni 884.09 mwaka 2010 hadi Sh trilioni 5.2 mwaka 2025, kutokana na usimamizi wa Sera ya Ushirikishwaji wa Wazawa.

Ameongeza kuwa wachimbaji wadogo sasa wanachangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini.

Mavunde ametaja hatua nyingine zilizochochea maendeleo ya sekta hiyo kuwa ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Utafiti wa Madini unaotengewa asilimia 10 ya mapato ya sekta hiyo kila mwaka kwa ajili ya utafiti, pamoja na kusainiwa kwa mikataba ya makubaliano ya mfumo wa uwekezaji (Mining Framework Agreements) na kampuni 14 za ubia kwa ajili ya kuendeleza miradi ya madini ya kinywee, nikeli, niobium, madini adimu ya ardhini (REE) na gesi ya helium.

Amesema Serikali pia imeimarisha masoko ya madini, upatikanaji wa vifaa, teknolojia, mitaji na taarifa za kijiosayansi kwa wachimbaji wadogo.

1003782596-1024x683 Mavunde:Sekta ya Madini yachangia 10.3% ya pato la taifa

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano huo Novemba 19, 2026, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuufunga Novemba 21.

Mkutano huo pia utakuwa na vikao vya mawaziri, mikutano ya kibiashara kati ya kampuni na kampuni (B2B), Kituo cha Pamoja cha Serikali, mafunzo ya uongezaji thamani na maonesho yatakayoonesha mnyororo mzima wa thamani wa madini kuanzia uchimbaji hadi uzalishaji wa bidhaa za mwisho.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Usiku wa Madini utakaohusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *