TOSCI yahamasisha matumizi ya mbegu bora, kukuza kilimo biashara, masoko ya kimataifa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

MATUMIZI ya mbegu bora yameelezwa kuwa nguzo muhimu ya kufanikisha ajenda ya kilimo biashara nchini na kuongeza uzalishaji wenye tija utakaowezesha Tanzania kuendelea kujitosheleza kwa chakula na kunufaika na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo taasisi hiyo inashiriki kupitia banda la Wizara ya Kilimo.

Chimagu amesema msingi wa kilimo biashara unaoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unaanzia kwenye matumizi ya mbegu bora zilizothibitishwa, kwasababu ndizo zinazowezesha wakulima kupata mavuno mengi, yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya soko.

1-6 TOSCI yahamasisha matumizi ya mbegu bora, kukuza kilimo biashara, masoko ya kimataifa

“Serikali imeendelea kusisitiza kilimo biashara, na msingi wa kilimo biashara ni matumizi ya mbegu bora. Sisi kama TOSCI jukumu letu ni kuhakikisha mbegu zote zinazowafikia wakulima zimehakikiwa na kuthibitishwa ubora wake,” amesema Chimagu.

Ameeleza kuwa TOSCI ndiyo taasisi yenye jukumu la kusajili aina mpya za mbegu nchini baada ya kupitia majaribio mbalimbali yanayothibitisha ubora wake, uwezo wa kuzalishwa katika maeneo tofauti ya Tanzania na sifa zake za kilimo.

Mbali na kusajili mbegu hizo, alisema taasisi hiyo pia husajili wazalishaji wa mbegu na mashamba yanayozalisha mbegu, huku ikifanya ukaguzi katika hatua zote za uzalishaji ili kuhakikisha mbegu zinabaki na ubora uliokusudiwa kabla ya kuwafikia wakulima.

“Tunafanya ukaguzi kuanzia shambani hadi maabara ili kuhakikisha mbegu zote zinakidhi viwango vya ubora. Tunachukua sampuli na kufanya uchunguzi kuhakikisha mbegu hizo zina sifa zilizosajiliwa,” amesema.

Aidha, Chimagu amesema TOSCI imeweka mfumo wa kidijitali unaowezesha mkulima kuthibitisha uhalali wa mbegu kabla ya kuzinunua.

Amefafanua kuwa kila mbegu halali lazima iwe imefungashwa na iwe na lebo maalumu ya TOSCI, huku akisisitiza kuwa ni kinyume cha sheria kuuza mbegu ambazo hazijafungashwa.

“Mbegu zote zinazouzwa lazima ziwe kwenye kifungashio. Ni marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu kuuza mbegu ambazo hazijafungashwa kwa sababu kifungashio kina taarifa zote muhimu za mbegu pamoja na lebo ya uthibitisho wa TOSCI,” amesema.

Amesema mkulima anaweza kuhakiki uhalali wa mbegu kwa kutumia simu ya mkononi kupitia mfumo wa 14852#, ambapo akiingiza namba iliyopo kwenye lebo atapata majibu yanayoonesha kama mbegu hiyo ni halisi au si halisi.

“Ukipata taarifa kuwa mbegu ni halisi, ujue imepitia taratibu zote za uhakiki wa ubora. Ikiwa si halisi, tunawataka wananchi watoe taarifa mara moja ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika,” amesisitiza.

2-4 TOSCI yahamasisha matumizi ya mbegu bora, kukuza kilimo biashara, masoko ya kimataifa

Pia amewataka wananchi kutoa taarifa wanapobaini mbegu zenye shaka ili taasisi iweze kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine, Chimagu amesema Tanzania imejijengea uwezo mkubwa wa kuzalisha mbegu zinazokubalika kimataifa kutokana na uwepo wa maabara ya taifa yenye ithibati ya kimataifa, hali inayowezesha mbegu zinazozalishwa nchini kuuzwa katika masoko mbalimbali ya nje.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye maabara ya mbegu inayotambulika kimataifa. Hii inatupa fursa ya kuzalisha na kuuza mbegu zetu katika masoko ya kimataifa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika duniani,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia Maonesho ya Sabasaba, TOSCI inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora, uzalishaji wa mbegu, biashara ya mbegu na fursa za kuuza mbegu ndani na nje ya Tanzania.

Chimagu aliwahimiza wananchi, wawekezaji na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la TOSCI ili kupata elimu kuhusu teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora na namna ya kushiriki katika biashara hiyo, akisema hatua hiyo itaongeza tija katika sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *