RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

• Yaweka mkakati wa kuimarisha uandishi unaowakilisha mahitaji na changamoto za wananchi wa vijijini

• Bulaya ataka kurejeshwa kwa ushindani wa kitaaluma, ubunifu na habari za kiuchunguzi

• Meena ataka waandishi na Serikali kujenga ushirikiano katika upatikanaji wa taarifa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) kimeweka mkakati wa kuhakikisha changamoto, mahitaji na mafanikio ya wananchi wa vijijini yanapata nafasi katika majukwaa makubwa ya habari.

Katibu Mkuu wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema hayo leo Oktoba 31, 2026 jijini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu na Kongamano la mwaka la tathmini ya huduma za habari na Mawasiliano vijijini.

1003584619-1024x682 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 na waandishi 20 waliokutana Dodoma baada ya kujifunza mifumo ya uandishi wa habari za vijijini katika nchi nyingine na kubaini umuhimu wa Tanzania kuwa na taasisi maalumu inayosimamia eneo hilo.

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuachana na uandishi unaotegemea mikutano na taarifa kwa vyombo vya habari na badala yake kwenda kwa wananchi kutafuta habari zenye matokeo.

1003584612-1024x808 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Kwigize amesema moja ya malengo makuu ya chama hicho ni kuondoa mtazamo unaoyapa kipaumbele zaidi maeneo ya mijini katika kuripoti habari, akisisitiza kuwa habari za vijijini zina thamani sawa na za mijini kwa sababu maendeleo ya maeneo hayo yanategemeana. 

Amesema RUJAT inalenga kukuza uandishi unaozingatia maadili, usio na ubaguzi na unaojumuisha makundi mbalimbali ya jamii, kiendeleza kujenga uwezo wa wanachama kupitia mafunzo, matumizi ya majukwaa ya kidijitali na programu za utetezi wa uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa. 

1003584622-1024x554 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Pia imepanga kuanzisha tuzo maalumu kwa waandishi watakaofanya vizuri katika kuandika habari za vijijini, kwa kuzingatia ubora wa kazi na namna wanavyotumia vyanzo kutoka katika jamii husika.

Amesisitiza kuwa waandishi wanapaswa kutoka katika utegemezi wa taarifa za mikutano na matukio na kwenda kutafuta sauti za wananchi, kuchunguza changamoto zao na kufuatilia matokeo ya mipango ya maendeleo. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bunda(CCM), Esther Bulaya, ameitaka tasnia ya habari kurejesha ubora wa uandishi uliokuwepo zamani, akisema ushindani wa kitaaluma, bidii, ubunifu na uchunguzi ndivyo vilivyojenga waandishi mahiri. 

1003584623-1024x831 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Ameeleza kuwa uzoefu wake katika vyombo vya habari vya Uhuru na Mzalendo ulimfundisha kuipenda taaluma na kufanya kazi kwa bidii, huku akitaja umuhimu wa kujifunza kutoka kwa waandishi wabobezi waliomjenga katika safari yake ya uandishi. 

Amesema ushindani aliokuwa nao na waandishi wenzake uliwafanya kujituma kutafuta habari bora na za kipekee, tofauti na hali anayoiona sasa ambayo inahitaji kutathminiwa.

1003584603 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Bulaya amesema aliwahi kufanya habari za kiuchunguzi kuhusu mimba za utotoni katika Wilaya ya Liwale na watoto wenye umri chini ya miaka 14 waliokuwa wakienda kwenye vilabu nyakati za usiku, akisisitiza kuwa mwandishi hapaswi kuishia kuripoti matukio ya kawaida bali kuwa na uwezo wa kuona masuala yanayohitaji kuchunguzwa na kuandikwa kwa kina. 

Ameeleza kuwa taaluma ya habari imemjengea ujasiri na kujiamini hadi kufikia nafasi ya ubunge, ambako ameshinda kwa mihula minne mfululizo kupitia vyama viwili tofauti. Aliahidi kuendelea kushirikiana na RUJAT katika juhudi za kuimarisha habari za vijijini.

Aidha Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinalenga kuwajengea waandishi uwezo wa kuripoti masuala ya vijijini kwa uelewa mpana wa maana ya jamii hizo, akieleza kuwa kijiji hakipaswi kutazamwa kwa eneo lake pekee, bali watu na shughuli zao. 

1003585026 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Amesema waandishi wanapaswa kujifunza namna ya kuipa habari sura ya wananchi wanaohusika, badala ya kuishia kurudia taarifa zilizotolewa katika mikutano na mikutano na waandishi wa habari.

Meena ametoa wito kwa taasisi za Serikali na wasemaji wake kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari kwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa, akisisitiza kuwa wanahabari si maadui wa Serikali bali ni wadau wanaoweza kufanya kazi pamoja katika kuhabarisha wananchi. 

Amesema wakati mwingine waandishi hukutana na vikwazo wanapotafuta ufafanuzi wa masuala ya umma, hivyo ni muhimu watendaji kuelewa majukumu yao na kutoa taarifa kwa wakati.

1003584611-1024x605 RUJAT yataka sauti za vijijini kutawala majukwaa ya habari

Amesisitiza kuwa RUJAT inalenga kujenga tasnia yenye waandishi wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kuibua masuala yanayogusa wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *