.Asema wanahabari wanapaswa kusimamia mahitaji ya wananchi bila kuongozwa na ajenda binafsi
• Ataka utafiti kubaini sababu za kupungua kwa ushawishi wa vyombo vya habari
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari kutowaachia wanaharakati jukumu la kuhabarisha umma, akisisitiza kuwa wajibu huo ni wa wanahabari wanaopaswa kusimamia mahitaji ya wananchi kwa kuzingatia weledi.
Amesema tofauti na wanaharakati ambao wanaweza kuwa na ajenda maalumu, mwandishi wa habari anapaswa kutekeleza wajibu wake wa kitaaluma kwa kuzingatia maslahi ya wananchi, hivyo kuachia makundi mengine kuchukua nafasi hiyo kunaweza kupunguza umuhimu wa taaluma ya habari katika jamii.

Msigwa ameyasema hayo leo, Oktoba 31,2026 jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu na Kongamano la mwaka la tathmini ya huduma za habari na Mawasiliano vijijini nchini Tanzania lililofanywa na Chama Cha Waandishi wa Habari Vijijini(RUJAT).
Amewataka Wanahabari hao kufanya utafiti kubaini sababu zinazowafanya wananchi kupunguza ufuatiliaji wa vyombo vya habari na kuelekeza usikivu wao kwenye makundi ambayo si jukumu lake la msingi kuhabarisha umma.

“Tusipokubali jukumu la kitaaluma la wanahabari lifanywe na wanaharakati tunapoteza umuhimu wetu na tunawanyima haki sahihi wananchi,” amesema.
Amesema ni muhimu kwa wanahabari kurejesha nafasi yao katika jamii kwa kuandaa habari zinazogusa maisha ya wananchi na kuibua changamoto zinazohitaji kutatuliwa.

Msigwa pia ameipongeza RUJAT kwa kuanzisha jukwaa la kuimarisha upatikanaji wa habari za vijijini, akieleza kuwa takribani asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini, huku zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya habari vikiwa mijini kwa mujibu wa takwimu za miaka mitano iliyopita.
Amesema hali hiyo imechangia wananchi wengi wa vijijini kutopata habari zinazohusu mazingira na mahitaji yao, hivyo akawataka waandishi kutumia jukwaa hilo kuwafikia wananchi hao.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari na waandishi, ambapo alibainisha udhaifu wa kiuchumi unaweza kuathiri uhuru na weledi wa mwandishi kwa kumlazimisha kutegemea fedha kutoka kwa watu au taasisi zenye maslahi maalumu.
Amewataka wadau kufanya utafiti na kuandaa mipango mahsusi ya kuimarisha uchumi wa sekta hiyo ili kuwawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na kusimamia maslahi ya wananchi.
Akizungumzia wajibu wa wanahabari katika kulinda nchi, Msigwa amewataka kutumia kalamu zao kwa uwajibikaji na kubadilisha kuwa taarifa zinaweza kutumiwa kujenga au kuumizana katika dunia ya sasa.

“Tunayo nchi ya kuilinda kupitia kalamu zetu. Tunaweza kutofautiana kwa namna yoyote ile, lakini tusitofautiane kwenye kulinda nchi yetu kupitia kalamu zetu,” amesisitiza.
Kuhusu ushirikiano wa Serikali na sekta ya habari, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari, akibainisha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini waandishi na kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari.