Dkt. Ligwanda: Elimu ya Amali ni msingi wa nguvu kazi ya Taifa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), limesema elimu ya amali na ufundi inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa, hatua inayochochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akizungumza kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, alisema baraza hilo limetumia maonesho hayo kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.

“Nachukua fursa hii kwanza kuwakaribisha wanahabari lakini pia jamii yote katika maonesho haya ya Sabasaba katika banda letu la NACTVET. Mwaka huu tunashiriki kwa mara nyingine na tumekuja kutumia fursa hii kufikisha ujumbe na kufikisha huduma kwa karibu zaidi katika jamii yetu,” amesema.

2-2-2-1024x576 Dkt. Ligwanda: Elimu ya Amali ni msingi wa nguvu kazi ya Taifa

Amesema wananchi wanaotembelea banda la NACTVET wanapata huduma zote zinazotolewa na baraza hilo, ikiwemo ushauri kuhusu uanzishwaji wa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na huduma nyingine za kitaalamu.

“Mwitikio nimeona ni mzuri sana. Takwimu zetu zinaonesha hadi sasa tumetembelewa na wageni wa kutosha kabisa. Naamini kupitia hao wamepata huduma walizokuwa wanahitaji na wanaweza kufikisha ujumbe kwa wengine kwamba tuko hapa Sabasaba na tunaendelea kutoa huduma,” amesema.

Dkt. Lingwanda amesema mwaka huu, NACTVET imeongeza eneo la wanafunzi wa shule za amali kuonesha kwa vitendo ujuzi walioupata darasani, hatua inayodhihirisha matokeo ya elimu inayotolewa.

“Vijana wetu wanaonyesha uwezo wao hapa, ina maana wamejifunza kwa vitendo na wanaweza kufanya. Tunategemea vijana kama hawa wakitoka hapa wana uwezo wa kufanya kazi kabisa. Kwa hiyo tunatengeneza nguvu kazi ya taifa yenye kujua namna ya kutekeleza majukumu mbalimbali,” amesema.

Amefafanua kuwa fani zilizooneshwa ni sehemu ndogo tu ya programu nyingi zinazoratibiwa na NACTVET, huku akieleza kuwa maonesho yajayo yatahusisha fani nyingine zaidi.

Kutokana na hilo, amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule za amali ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujitegemea, huku akiwakaribisha pia wawekezaji wenye nia ya kuanzisha shule hizo kufika banda la NACTVET kupata maelezo ya taratibu zinazotakiwa.

3-3-3-1024x576 Dkt. Ligwanda: Elimu ya Amali ni msingi wa nguvu kazi ya Taifa

“Ujumbe kwenye hili ni kuhamasisha kwanza wazazi kupeleka watoto wetu kwenye kujifunza mafunzo ya amali, lakini pia wale wenye uwezo wa kuanzisha taasisi za sekondari zinazoweza kutoa mafunzo ya amali tunawakaribisha hapa tuweze kuwaelezea kuhusu utaratibu na hatimaye waanzishe,” amesema.

Akizungumzia mchango wa elimu ya ufundi katika maendeleo ya taifa, Dkt. Lingwanda amesema wahitimu wa elimu hiyo wameendelea kuzalisha bidhaa, kujiajiri, kuajiriwa na kubuni teknolojia mbalimbali zinazochochea ukuaji wa uchumi.

“Tunatengeneza nguvu kazi ambayo itaweza kutengeneza bidhaa, kufanya biashara kwa sababu kuna masomo ya biashara pia, na nguvu kazi ambayo inaweza kubuni. Kwa hiyo mchango kwa kweli ni mkubwa,” amesema.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa, ukuaji wa viwanda na uundaji wa ajira.

“Mtazamo wangu ni kwamba kama nchi tunafanya vizuri, tuko kwenye hatua nzuri. Naona mwamko, naona bidhaa za kwetu zikiwa zimetengenezwa humu maana yake kuna uzalishaji wa kutosha, biashara zinafanyika, ajira zinatengenezwa ambayo ndiyo dira yetu inatuelekeza. Tutilie mkazo kwenye haya ambayo tayari yameonesha kufanya vizuri kama taifa litasonga mbele,” amesema.

4-4-4-1024x576 Dkt. Ligwanda: Elimu ya Amali ni msingi wa nguvu kazi ya Taifa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *