Serikali yaendelea kuwekeza kujenga ujuzi wa Watanzania kukidhi soko la ajira

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Dkt. Evaline Munisi, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya ujuzi ili kuandaa wataalamu wa kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inazalisha wataalamu wake wenyewe wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira linaloendelea kukua.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Munisi alisema ameridhishwa na namna watumishi wanavyotoa huduma kwa wananchi kwa weledi, ubunifu na kujituma.

Alisema katikati maonesho hayo alitembelea banda la Idara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, ambako alishuhudia watumishi wakitoa elimu kuhusu masuala ya kazi, afya na usalama mahali pa kazi, sheria za kazi pamoja na miongozo ya mishahara ya sekta mbalimbali.

2-13 Serikali yaendelea kuwekeza kujenga ujuzi wa Watanzania kukidhi soko la ajira

“Elimu hii inasaidia kuwaondolea wananchi manung’uniko na malalamiko kwa kuwa wanapata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu kazi na ajira,” alisema.

Katika eneo la mahusiano kazini, Dkt. Munisi alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kijamii, zikiwemo taasisi za dini, vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia kwa lengo la kuimarisha mshikamano na ushirikiano katika jamii.

Alisema mahusiano mazuri ni msingi muhimu wa maendeleo na akatoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano.

Aidha, alisema alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali ikiwemo NSSF, WCF, OSHA na PSSSF, ambako alijionea wananchi wakipata huduma na elimu kuhusu masuala yanayowahusu.

Alibainisha kuwa PSSSF imeboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya kidijitali kupitia meza maalumu inayomwezesha mwananchi kuona taarifa zake za mafao na huduma nyingine papo hapo.

3-13 Serikali yaendelea kuwekeza kujenga ujuzi wa Watanzania kukidhi soko la ajira

Dkt. Munisi alisema pia alitembelea banda la Idara ya Sera, Bunge na Wenye Ulemavu pamoja na mabanda ya taasisi nyingine za Serikali, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa ya maonesho hayo kupata elimu na huduma zinazowagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *