
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limejivunia kupata faida ya takribani Sh bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25, mafanikio ambayo yamechangiwa na maboresho ya uendeshaji wa shirika pamoja na kuongezeka kwa mapato na wateja.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema matarajio ya shirika ni kuongeza faida hiyo zaidi katika mwaka wa fedha 2025/26 kupitia uwekezaji katika teknolojia za kisasa na upanuzi wa huduma za mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Marwa alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuliendesha TTCL kwa misingi ya kibiashara.
“TTCL ilipata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25, na matarajio yetu ni kuongeza zaidi faida hiyo katika mwaka wa fedha 2025/26 kutokana na ukuaji wa mapato na kuongezeka kwa wateja,” alisema.
Alisema sambamba na mafanikio hayo, TTCL inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kuonesha huduma mbalimbali za kidijitali zinazotolewa kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Marwa alisema huduma hizo ni Sifa Soni, inayotoa intaneti ya kasi kubwa kwa gharama nafuu, pamoja na FTTx Experience Centre, inayowawezesha wananchi kujionea matumizi ya intaneti katika nyumba janja (Smart Home), ikiwemo mifumo ya usalama, vifaa vinavyounganishwa na intaneti na huduma za burudani.
Aidha, alisema shirika linaendelea kuonesha huduma za National ICT Data Centre (NIDC), zikiwemo huduma za cloud computing zinazowasaidia wateja kuhifadhi taarifa zao kwa usalama bila gharama kubwa za kujenga miundombinu yao wenyewe.
Marwa alisema TTCL itaendelea kupanua huduma zake, kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuboresha huduma za mawasiliano ili kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
