
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imemtunuku mwanachama wa Dream Team Explorers, Khalid Hamadal Baruani, Cheti cha Balozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuitangaza Tanzania kupitia safari ya kihistoria ya barabarani kutoka Oman hadi Tanzania pamoja na kutembelea karibu asilimia 90 ya vivutio vya utalii nchini.
Cheti hicho kilikabidhiwa kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mafuru alisema serikali imeweka utaratibu wa kutambua na kuwapongeza watu binafsi na taasisi zinazochangia kuitangaza Tanzania duniani, ili kuongeza nguvu katika kampeni za kukuza sekta ya utalii.
“Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, tumemkabidhi Bwana Khalid Baruani Cheti cha Balozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania ili kutambua mchango wake mkubwa wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii.
“Safari yake ya kutoka Oman kupitia zaidi ya nchi 10 hadi Tanzania na kuzunguka karibu asilimia 90 ya vivutio vya utalii imekuwa mfano wa uzalendo na ubunifu katika kuitangaza nchi yetu,” amesema Mafuru.
Amesema TTB itaendelea kushirikiana na mabalozi wa hiari wa utalii pamoja na wadau wengine wanaojitolea kuitangaza Tanzania katika nchi mbalimbali.

“Tunawahimiza Watanzania wanaofanya kazi kubwa ya kuitangaza sekta ya utalii kujitokeza. Tuko tayari kuwashirikisha na kuwapa heshima ya kuwa Mabalozi wa Hiari wa Utalii ili kwa pamoja tuendelee kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza utalii,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mafuru amesema Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake zote za uhifadhi, elimu na utalii zinaendelea kushiriki Maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kuonesha mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa na kutoa elimu kwa wananchi.
Amesema banda la wizara limekusanya taasisi zote muhimu za sekta hiyo, zikiwemo TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Makumbusho ya Taifa, Chuo cha Taifa cha Utalii pamoja na vyuo vya uhifadhi kutoka Arusha, Moshi, Iringa na Mwanza.
Mafuru amesema wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kujionea matangazo ya moja kwa moja kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, kupata ofa za safari za utalii, kujisajili katika vyuo vya utalii na uhifadhi pamoja na kupata taarifa mbalimbali kuhusu vivutio vya Tanzania.
Aidha, amesema TTB inaendelea kufanya majaribio ya mfumo mpya wa kidijitali wa Booking Destination Portal, utakaowawezesha watalii kupanga safari zao mapema kwa kuchagua hoteli, kampuni za utalii, vivutio na kufanya malipo kabla ya kuwasili nchini.
Mafuru amesema mfumo huo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuongeza ushindani wa sekta ya utalii katika soko la kimataifa.
Pia amesema Tanzania inaendelea kujiandaa kupokea matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo michuano ya AFCON, mkutano wa mabunge duniani utakaofanyika Arusha pamoja na mashindano ya urembo ya dunia, ambayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya wageni na mapato ya sekta ya utalii.
Amewataka Watanzania kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu, kujionea vivutio mbalimbali na kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo inayozidi kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa.

Baada ya kupokea cheti hicho, Baruani amesema heshima hiyo ni deni kwake la kuendelea kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa, hususan nchi za Ghuba ambazo zina idadi kubwa ya watu wanaopenda utalii wa mazingira na wanyamapori.
“Ninashukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona na kufuatilia safari yetu.
Pia nawashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania ambao waliamini wazo letu tangu mwanzo na kutuunga mkono katika juhudi za kuitangaza Tanzania nje ya nchi,” alisema.
Baruani amesema safari yao ilianza Oman na kupitia zaidi ya nchi 10 kabla ya kuingia Tanzania, ambapo walizunguka maeneo mengi ya utalii kwa lengo la kuonesha uzuri wa vivutio vya Tanzania kwa dunia.
Amesema gari waliyotumia katika safari hiyo imebeba historia kubwa, jambo lililomsukuma kuikabidhi kama zawadi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Niliona gari hii ina historia kubwa. Imepita nchi nyingi na imezunguka karibu Tanzania nzima ikitangaza utalii. Nimeamua kumkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kuutangaza utalii wa Tanzania duniani.
Nilichokuwa nafanya mimi, yeye amekifanya kwa kiwango kikubwa zaidi akiwa Rais wa nchi.”
Amesema mchango wa Rais Samia katika kuutangaza utalii umeifanya Tanzania kuandika historia mpya ya mafanikio ya sekta hiyo.
“Rais Samia alisimama mwenyewe kuutangaza utalii wa Tanzania. Leo tunaona matokeo yake kupitia ongezeko la watalii na mapato ya sekta. Historia hiyo haijawahi kutokea,”amesema.
Baruani amesema ataendelea kuitangaza Tanzania kwa kutumia lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu ili kufikia masoko mapya ya utalii.
“Nchi za Ghuba zinapenda vivutio vya asili kuliko vya kutengenezwa. Tanzania imebarikiwa kuwa na hifadhi za wanyamapori, bahari, uwindaji wa kitalii na vivutio vingi vya asili. Hayo ndiyo tutakwenda kuyatangaza zaidi,”amesema.
Ameongeza kuwa Dream Team Explorers itaendelea kutumia magari ya aina ya 4×4 yenye namba za usajili wa nchi za Kiarabu kama sehemu ya mkakati wa kuvutia watu wengi kufuatilia safari zao na kupata hamasa ya kutembelea Tanzania.
Aidha, amesema kampeni zijazo zitawalenga pia Watanzania ili wajifunze kutembelea na kuthamini vivutio vyao.
“Sio wageni pekee wanaopaswa kutembelea vivutio vya utalii. Watanzania pia wanapaswa kuvitambua na kuvifurahia kwa sababu Mwenyezi Mungu ametubariki kwa rasilimali nyingi za kipekee.”
