TCAA yasogeza huduma za dawati maalumu karibu na wananchi

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi na wadau wa sekta ya usafiri wa anga kupitia Dawati Maalum la Huduma kwa Wateja, likiwa na lengo la kuhakikisha wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati.

Akizungumza katika Banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam(Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja wa TCAA, Rashid Mngoya, amesema dawati hilo limeanzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka.

Mngoya amesema kupitia dawati hilo, wateja na wadau wanaweza kupata ufafanuzi kuhusu huduma za TCAA, kuwasilisha maoni, hoja na changamoto, pamoja na kuelekezwa kuhusu taratibu mbalimbali zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.

2-22-1024x691 TCAA yasogeza huduma za dawati maalumu karibu na wananchi

Ameeleza kuwa Dawati la Huduma kwa Wateja ni sehemu muhimu ya jitihada za TCAA za kuwa karibu zaidi na wateja wake na kuhakikisha masuala yanayowasilishwa yanapokelewa, kufanyiwa kazi na kupatiwa majibu kwa wakati.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati. Dawati hili linatoa fursa kwa wananchi na wadau kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka na kupata msaada kuhusu huduma wanazozihitaji,” amesema Mngoya.

Ameongeza kuwa TCAA imejipanga kuendelea kuisimamia sekta ya usafiri wa anga kwa weledi na ufanisi, huku ikihakikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama, ulinzi na ubora wa huduma vinazingatiwa.

Awali akizungumzia maboresho mengine yanayotekelezwa na Mamlaka, Meneja Uhusiano wa TCAA, Ally Changiwa, amesema TCAA imeendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano na utoaji wa taarifa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wadau.

Changiwa amesema miongoni mwa maboresho hayo ni tovuti ya TCAA, ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ikiwa imeongezewa taarifa nyingi zaidi, hatua inayolenga kuwezesha watumiaji wengi zaidi kupata taarifa kwa urahisi.

Ameongeza kuwa tovuti hiyo pia imeboreshwa kwa kuwekwa sehemu ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara, ambayo inatoa majibu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kusimamiwa na TCAA.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, TCAA imeendelea kutoa elimu na ufafanuzi kwa wananchi kuhusu majukumu yake, huduma za kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege nyuki, pamoja na masuala mengine yanayohusu sekta ya usafiri wa anga.

Ushiriki huo unaakisi dhamira ya TCAA ya kuimarisha mawasiliano na wadau, kuongeza uelewa wa umma na kuendelea kutoa huduma zinazochangia usalama, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga nchini.

4-8-1024x682 TCAA yasogeza huduma za dawati maalumu karibu na wananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *