
Gugange ataka halmashauri kudhibiti ujenzi holela, kulinda maeneo ya wazi na kusimamia matumizi ya ardhi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imeonya kuhusu kuendelea kwa ujenzi holela jijini Dar es Salaam, ikieleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya maeneo ya jiji hilo hayajapangwa vizuri, hali inayochangia changamoto za miundombinu, usafiri na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, ametoa maelekezo saba kwa halmashauri nchini kuhakikisha zinaboresha upangaji na uendelezaji wa miji ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na ukuaji wa miji usiozingatia mipango.
Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Majiji Duniani, amesisitiza kuwa halmashauri zinapaswa kuandaa mipango inayozingatia uwezo wa bajeti zake ili iweze kutekelezwa kwa vitendo.
Amezitaka halmashauri kuweka kipaumbele katika urasimishaji wa makazi, ujenzi wa barabara na mifereji ya maji ya mvua, masoko, usafi wa mazingira na huduma za kijamii. Pia amesisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kusimamia miradi, pamoja na kuimarisha mifumo ya kupokea na kushughulikia malalamiko.
Maelekezo mengine ni kulinda maeneo ya wazi, hifadhi za barabara na mikondo ya maji, kuandaa miradi inayoweza kuvutia uwekezaji na ubia wenye maslahi kwa umma, kuimarisha usimamizi wa ardhi na vibali vya ujenzi, pamoja na kutoa taarifa za wazi kuhusu bajeti na utekelezaji wa miradi.
Akieleza ukubwa wa changamoto hiyo, amesema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu milioni 61.7, ambapo asilimia 34.9 waliishi mijini, hali inayoongeza umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na miundombinu.
Amesema hata miji inayokua kwa kasi, ikiwamo Dodoma, inapaswa kuhakikisha maeneo yanapangwa kabla ya kuendelezwa ili kuepuka msongamano wa makazi, foleni na upungufu wa huduma muhimu.
Akizungumzia mafanikio ya Serikali katika eneo hilo, amesema hadi mwaka 2026, mamlaka 28 za serikali za mitaa zilikuwa zimeandaa mipango kabambe iliyoidhinishwa tangu mwaka 2016, huku mipango ya kina zaidi ya 10,000 ikiandaliwa na nyaraka 675 za umiliki wa ardhi kutolewa.
Ameongeza kuwa maeneo 111 katika mikoa 24, yenye ukubwa wa takribani hekta 24,000, yametambuliwa kwa ajili ya uendelezaji upya.
Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu na Ushindani wa Miji Tanzania (TACTIC), wenye mkopo wa Dola za Marekani milioni 278, unaolenga kuboresha miundombinu katika miji 45 yenye wakazi takribani milioni 5.5.
Amesema miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara, masoko, vituo vya mabasi, maegesho, madampo na mifereji ya maji ya mvua, huku Serikali ikiendelea kusimamia ubora wa miradi na matumizi sahihi ya fedha.
Katika hatua nyingine, ameagiza halmashauri kudhibiti ubora wa vifaa vya ujenzi, hususan matofali, ili kuhakikisha wananchi wanatumia vifaa vinavyokidhi viwango na kujenga makazi salama.
Pia amehimiza kulindwa kwa maeneo ya wazi kwa manufaa ya mazingira na afya za wananchi, pamoja na matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme na gesi ili kupunguza gharama za uendeshaji na uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Lawrence Mlacky, amesema manispaa hiyo imeanza hatua za kupanga upya eneo la Sinza kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, baada ya mpango huo kupitia vikao vya wataalamu na kuidhinishwa na Baraza la Madiwani.
Amesema pia manispaa hiyo imetenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa masoko na vituo vya mabasi, huku akihimiza ushirikiano wa wananchi na sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji.



