Halmashauri zatakiwa kutumia fursa za PPP

1003605548 Halmashauri zatakiwa kutumia fursa za PPP

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Mvomero, Sara Msafiri, amezitaka Halmashauri na mamlaka za serikali kuonesha hatua zilizochukua katika kuandaa miradi itakayotekelezwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), akieleza kuwa licha ya maelekezo ya Serikali na Bunge, bado hakuna maendeleo yanayoonekana katika utekelezaji wake.

Msafiri amesema katika Bunge la Bajeti lililopita, Serikali na Bunge zilikubaliana kila mamlaka ya serikali iandae angalau mradi mmoja na kila halmashauri iandae angalau miradi mitatu kwa ajili ya kutekelezwa kupitia mfumo wa PPP, lakini hadi sasa maandiko ya miradi hiyo hayajaonekana kuwasilishwa.

Akichangia tathmini ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika vikao vya Bunge vinavyoendelea jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, mbunge huyo amesema utekelezaji wa mipango iliyoidhinishwa unahitaji uwajibikaji wa taasisi husika, badala ya kuishia katika maelekezo na makubaliano.

“Serikali ilishaelekeza na Bunge tukaridhia kwamba halmashauri zote ziandae angalau miradi mitatu kwa ajili ya utekelezaji kupitia PPP,” amesema.

Amemuuliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maelekezo hayo, akieleza kuwa ufuatiliaji wake umebaini kutokuwapo kwa maandiko ya miradi ya PPP yaliyowasilishwa na halmashauri au mamlaka za serikali.

Msafiri amehoji sababu za taasisi hizo kuendelea kuandaa miradi inayotegemea fedha za bajeti ya Serikali, kodi na mikopo, huku maandalizi ya miradi inayoweza kutekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi yakiwa hayaonekani.

“Mamlaka za serikali zimekuwa zikitenga fedha nyingi kwa ajili ya kuandika maandiko ya miradi inayotegemea fedha za serikali, mikopo au kodi. Kama fedha za kuandaa miradi hiyo zinapatikana, kwa nini maandiko ya miradi ya PPP hayaandaliwi?” amehoji.

Akitaja maeneo yanayoweza kunufaika na mfumo huo, Msafiri alitaja ujenzi wa nyumba za watumishi wa serikali za mitaa, akisema licha ya uwekezaji unaofanyika katika vituo vya afya, zahanati na shule, changamoto ya makazi ya watumishi bado ni kubwa.

Amesema kila halmashauri ina angalau watumishi 2,000, jambo linaloonesha mahitaji makubwa ya nyumba za makazi ambayo yanaweza kukidhiwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

“Katika miradi ya vituo vya afya, zahanati, shule na mingine, kumetengwa maeneo ya kujenga nyumba za watumishi. Kwa nini miradi hii isifanyike kupitia PPP?” amehoji.

Katika hatua nyingine, Msafiri amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Mwalimu Nyerere na uboreshaji wa bandari.

Amesema miundombinu hiyo inapaswa kuwa kichocheo cha uwekezaji katika sekta nyingine, akieleza kuwa Bwawa la Mwalimu Nyerere halipaswi kuonekana kama mradi wa kuzalisha umeme pekee, bali pia liwe fursa ya kuendeleza umwagiliaji, usafiri wa majini na utalii.

“Tunataka kuona umwagiliaji, usafiri wa majini, utalii na shughuli nyingine zikiendelezwa pale. Nchi nyingine zina mamlaka zinazosimamia shughuli hizo katika miradi mikubwa kama hiyo,” amesema.

Kuhusu sekta ya barabara, alipendekeza Mamlaka ya Barabara Tanzania (TANROADS) ibadilishiwe muundo na kupewa hadhi ya mamlaka kamili yenye uwezo wa kusimamia miradi ya PPP, akitolea mfano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Amesema muundo wa sasa wa TANROADS una urasimu unaoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi, akitaja barabara ya Chalinze–Morogoro ambayo, kwa mujibu wake, imejadiliwa kwa zaidi ya miaka mitano bila utekelezaji wa maana kupitia mfumo wa PPP.

Aidha Msafiri amesema utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa hauwezi kutegemea mikopo na bajeti ya ndani pekee, hivyo halmashauri na mamlaka za serikali zinapaswa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na kutumia fursa za uwekezaji wa sekta binafsi.

Amemtaka Profesa Mkumbo kutoa mrejesho Bungeni kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo au kueleza njia mbadala za kupata fedha za maendeleo iwapo mfumo wa PPP unakabiliwa na vikwazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *