
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kilichotokea usiku wa Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es
Salaam.
Katika taarifa ilyotumwa kwa vyombo vya habari leo Februari 20, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, imeeleza Rais Samia amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa.
Rais Dkt. Samia amesema anamkumbuka Kardinali Pengo kama kiongozi wa kiroho na mzalendo
aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano
wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

Ameongeza kuwa, Taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea,
na kwamba mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea
kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa.
Rais Dkt. Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Mhashamu Jude Thaddaeus
Ruwa’ichi, OFMCap, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini, pamoja na waumini wote
walioguswa na msiba huu mzito.
Aidha, Rais Dkt. Samia anaungana na Kanisa, waumini na Watanzania wote kwa
ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, na anamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe
roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina. Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe!
