
Na Mary Geofrey
SIMANZI na huzuni vimetawala kwa wanaumi wa Kanisa Katoliki ikiwa ni siku ya tatu ya Mfungo wa siku 40 za Kwaresma, baada ya habari kuenea kutoka ndani na nje ya Tanzania kuwa, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo, Katoliki la Dar es Salaam, Kardinali Pengo amefariki dunia.
Tamati ya utume wake duniani kwa kiongozi huyo mkubwa wa Kanisa Katoliki, ilifika jana Februari 19, 2026, majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 Kijiji cha Mwazye, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Nyanda za Juu Kusini jirani kabisa na Ziwa Tanganyika.
Alisomea Thiolojia ya Maadili mjini Roma katika Chuo Kikuu cha Pontifical Lateran, ambako alipata shahada ya uzamivu (udaktari) mwaka 1977.

Itakumbukwa kuwa mwaka 1971 alipata daraja lake la Upadri.
Alifundisha Thiolojia ya Maadili katika Seminari Kuu ya Kipalapala iliyo Tabora kwa muda mfupi, kisha akawa Gombera (Rector) wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea jijini Dar es Salaam hadi mwaka 1983.
Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea (sasa Lindi) mwaka 1983, na baadaye Askofu wa Tunduru–Masasi mwaka 1985.

Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi (Coadjuctor) Dar es Salaam, akingojea kustaafu rasmi kwa Laurean Kardinali Rugambwa.
Mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam kufuatia kustaafu kwa Kardinali Rugambwa ambaye alifariki dunia Desemba 1997.
Pengo alitangazwa kuwa Kardinali na Papa John Paul II katika mkutano wa makadinali (consistory) wa Februari 21, 1998.

Alikuwa miongoni mwa makardinali waliopiga kura katika mkutano wa kumchagua Papa mwaka 2005 uliomchagua Papa Benedict XVI na pia katika mkutano wa mwaka 2013 uliomchagua Papa Francis.
Alikuwa mwanachama wa vyombo mbalimbali vya Curia ya Vatican, ikiwamo uinjilishaji wa mataifa, mafundisho ya imani, mazungumzo ya kidini na tamaduni (mabaraza), pamoja na Baraza Maalum la Afrika la Sinodi ya Maaskofu.
Tangu mwaka 2007 alikuwa Rais wa SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar).
Septemba 18, 2012, aliteuliwa na Papa Benedict XVI kuwa mmoja wa wajumbe wa Sinodi kwa Mkutano Mkuu wa 13 wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu uliofanyika Oktoba 2012.
Papa Francis aliridhia ombi la Kardinali Pengo kustaafu uaskofu mkuu Agosti 15, 2019 na baadaye nafasi yake kuchukuliwa na Thaddaeus Ruwa’ichi.

Jana saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, Februari 19, 2026, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Tasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa Dar es Salaam Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, alitangaza kifo cha Kardinali Polycarp Pengo.
Itakumbukwa kuwa tayari Kardinali Pengo, alikwishaeleza bayana anapendelea azikwe eneo la Pugu, lililopo takribani Kilomita 25 nje ya jiji la Dar es Salaam.

Kardinali Pengo anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika uongozi wa kiroho, maadili ya jamii na maendeleo ya Kanisa Katoliki nchini.
Katika kipindi chake chote cha uongozi, alijulikana kwa msimamo thabiti katika masuala ya maadili, mshikamano wa kijamii na sauti ya hekima katika mijadala ya kitaifa.
Hata baada ya kustaafu uongozi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 2019, aliendelea kuwa mlezi wa kiroho na mshauri wa viongozi wa Kanisa pamoja na waumini.
Urithi wake unaendelea kubaki katika historia ya Kanisa na Taifa kama mfano wa uongozi wa imani, busara na huduma kwa jamii.
