PPP yatekeleza Miradi ya trilioni 8.6/- mwaka 2026/27

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI inaendelea kutumia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ambapo jumla ya miradi 10 yenye thamani ya Sh trilioni 8.6 ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika mwaka wa fedha 2026/27.

Miradi hiyo inahusisha sekta za usafirishaji, biashara na miundombinu, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Kwanza na ya Pili, unaolenga kuboresha huduma za usafiri wa mijini jijini Dar es Salaam.

1003666532 PPP yatekeleza Miradi ya trilioni 8.6/- mwaka 2026/27

Kupitia mradi huo, huduma za usafiri zinatarajiwa kuboreshwa kwa kupunguza msongamano wa magari, kuokoa muda wa wananchi na kuongeza ufanisi wa usafirishaji. Aidha, mfumo huo unatoa fursa kwa wawekezaji binafsi kuwekeza katika mabasi ya kisasa, vituo na mifumo ya tiketi za kidijitali.

Mradi mwingine ni ujenzi na uendeshaji wa Jengo la Biashara la DDC Kariakoo, unaolenga kuanzisha kitovu cha biashara katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Kupitia mfumo wa PPP, mwekezaji binafsi anajenga na kuendesha jengo hilo kwa kipindi fulani, huku Serikali ikipata mapato kupitia kodi na gawio. Mradi huo pia unatarajiwa kukuza biashara za ndani na kuongeza ajira kwa vijana.

1003666530 PPP yatekeleza Miradi ya trilioni 8.6/- mwaka 2026/27

Miradi mingine inayotekelezwa kwa mfumo huo ni uanzishwaji wa vituo vya ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto, uboreshaji wa uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ukarabati na uendeshaji wa Reli ya TAZARA.

Pia uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam unalenga kuongeza ufanisi wa shughuli za upakuaji na upakiaji wa mizigo, kutokana na umuhimu wake kama lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani.

Kwa upande wa Reli ya TAZARA, mradi wa ukarabati na uendeshaji wake unahusisha miundombinu muhimu ya usafirishaji wa shehena kati ya Tanzania na Zambia.

Aidha, orodha hiyo inajumuisha ujenzi wa kituo cha kisasa cha huduma za usafirishaji shehena chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambacho kinalenga kuboresha mnyororo wa usafirishaji wa mizigo nchini.

Kwa ujumla, miradi hiyo 10 yenye mtaji wa Sh trilioni 8.6 inaonesha nafasi ya sekta binafsi katika kushiriki utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kupitia mfumo wa PPP, ambao unaiwezesha Serikali kutekeleza miradi hiyo bila kutegemea fedha za bajeti pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *