Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Mkoa huo umepata mwekezaji kutoka Ghana atakayejenga kiwanda cha kuzalisha mbolea kwa kutumia taka, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa taka unaoukabili mkoa huo unaozalisha takribani tani 5,400 kwa siku.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza kiwango cha taka zinazochakatwa na kupunguza zinazobaki katika maeneo mbalimbali ya jiji, baada ya kubainika kuwa ni asilimia 60 tu ya taka zinazozalishwa hukusanywa na kupelekwa dampo, huku asilimia 40 zikibaki.

Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 06,2026, Mkuu huyo wa Mkoa amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya taka nchini.
Amesema Rais Samia ametoa maelekezo kwa Mkoa kuhakikisha ndani ya miezi mitatu kunakuwa na wawekezaji wanaojihusisha na uchakataji wa taka ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye manufaa.
Amesema tayari mkoa umepata mwekezaji kutoka Ghana atakayowekeza katika kiwanda cha kuzalisha mbolea kutokana na taka, huku kukiwa na fursa nyingine kwa wawekezaji kuingia katika mnyororo wa thamani wa taka.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kupunguza kiasi cha taka zinazobaki katika maeneo ya makazi na kuwezesha taka hizo kutumika kama malighafi katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wawekezaji wengine kujitokeza katika sekta hiyo ili kusaidia kuboresha usimamizi wa taka na kuifanya Dar es Salaam kuwa safi wakati wote.
Katika hatua nyingine, amesema Mkoa huo unatarajia kuzindua kampeni maalumu ya usafi Novemba 14, 2026, katika viwanja vya Posta, Kijitonyama, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutunza mazingira.
Amesema kampeni hiyo itatumia kaulimbiu isemayo, “Dar es Salaam safi inawezekana, tushiriki kwa pamoja,” huku siku ya uzinduzi ikitarajiwa kuhusisha zoezi la usafi na ugawaji wa vifaa kwa ajili ya shughuli hizo.

Amesema wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia vifaa vya usafi, akiwahimiza wengine kuendelea kujitokeza kuunga mkono kampeni hiyo.
Ameongeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kuimarisha usimamizi wa usafi katika mitaa 564 ya jiji kupitia wasimamizi watakaosaidia kuratibu shughuli za usafi na kuwabaini watu wanaochafua mazingira kwa makusudi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Katika kampeni hiyo pia kutakuwa na kliniki ya ardhi itakayowapa wananchi fursa ya kuwasilisha changamoto zao kuanzia saa tatu asubuhi, huku wataalamu wakisikiliza na kusaidia kuzitatua.
Pia, kutakuwa na huduma za afya za kawaida bila malipo pamoja na zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za mkoa kuunganisha wadau na wananchi katika kutatua changamoto za kijamii, huku akisisitiza kuwa usafi wa jiji unahitaji ushiriki wa kila mmoja.