
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewataka Wasimamizi wa Miradi iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kutekeleza kikamilifu miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi hiyo zinanufaika na kutatuliwa changamoto mbalimbali zilizopo katika maeneo yao.
Akiwa mkoani Mtwara hivi karibu, Ndejembi amesema kuwa miradi ya kusaidia jamii isibaki kuwa ile iliyoainishwa kwenye mikataba bali wataalam wanapaswa kujikita pia katika kusaidia shughuli za kijamii kulingana na mahitaji halisi ya wananchi, akitolea mfano wa ukarabati wa vyumba vya madarasa kwa kupiga rangi, kuweka vigae pamoja na kurekebisha miundombinu iliyoharibika kama pampu za maji.
Aidha, Waziri Ndejembi ameonesha shauku ya kuona jamii zilizo katika maeneo yanayotekelezwa miradi zinanufaika kwa kupata fursa mbalimbali ikiwamo za elimu akitolea mfano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC kusomesha wanafunzi wa Mtwara katika masuala ya Mafuta na Gesi ili kuwaandaa kuwa Wataalam wa Sekta hiyo siku zijazo.



