Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na mamlaka za Kenya imefanikiwa kuvunja mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
Hatua hiyo imefika baada ya kukamata shehena za heroin na methamphetamine pamoja na watuhumiwa saba wanaohusishwa na mtandao huo katika nchi hizo mbili.

Katika operesheni hizo, DCEA ilikamata paketi 299 za dawa za kulevya eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, zikiwemo paketi 24 za heroin na 275 za methamphetamine, kabla ya kushirikiana na mamlaka za Kenya kukamata paketi nyingine 454 za methamphetamine eneo la Kwale, Mombasa.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo leo Novemba 9, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema operesheni ya kwanza ilifanyika Novemba 6, 2026, ambapo dawa hizo zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo pia yanashikiliwa kutokana na kuhusishwa na uhalifu huo.

Amesema katika operesheni hiyo watuhumiwa wanne walikamatwa, akiwemo Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda, Issa Said Nassoro (34), Ibrahim Said Chembela (30) pamoja na Mohamed Ally Shemtuu (45), ambao ni wakazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Lyimo, baada ya kuhojiwa, watuhumiwa hao walieleza kuwa dawa hizo walizichukua Mombasa, Kenya na kuzisafirisha kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro, mkoani Tanga.

Kutokana na maelezo hayo, DCEA iliwasiliana na mamlaka husika nchini Kenya na kushirikiana kiutendaji kubaini chanzo cha dawa hizo, eneo lililotumika kuzihifadhi pamoja na kuwabaini wahusika wengine wa mtandao huo.
Ushirikiano huo ulizaa matokeo Novemba 7, 2026, baada ya DCEA kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB) kufanya operesheni eneo la Kwale, Mombasa, na kukamata paketi 454 za methamphetamine pamoja na watuhumiwa wengine watatu.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu Mbwiga, Seif Said Hamad (54), maarufu Babu Seif, wote raia wa Tanzania, na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda.
Lyimo amesema baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa ni vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya unaofanya shughuli zake katika nchi mbalimbali, zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.

Amesema miongoni mwa watuhumiwa wanaohusishwa na mtandao huo ni Saleh Khamis Baseleman, maarufu Mbwiga, ambaye anadaiwa kununua dawa za kulevya moja kwa moja nchini Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi fukwe za Mombasa, Kenya, kabla ya kuzisambaza katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.
Aidha, Baseleman anahusishwa na ukamataji wa dawa za kulevya tani 3.5 uliofanywa na DCEA Desemba 2023 katika eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Amesema kwa sasa, taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Lyimo amesema mafanikio ya operesheni hizo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukabiliana na dawa za kulevya, akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uwepo wa biashara na matumizi ya dawa hizo.