Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Afrika Mashariki katika Umoja wa Vyama vya Siasa Barani Afrika (African Political Parties Initiative – APPI), hatua inayokipa chama hicho nafasi ya kushiriki katika kuimarisha ushirikiano wa kisiasa barani humo.
Dkt. Migiro amechaguliwa katika Mkutano wa Pili wa Vyama vya Siasa Barani Afrika (African Political Parties Summit), uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, uliofanyika Novemba 5 hadi 7, 2026, uliowakutanisha wawakilishi wa vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Katika mkutano huo, Dkt. Migiro aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, aliyeshiriki majadiliano kuhusu nafasi ya vyama vya siasa katika kuimarisha utawala, ushirikiano wa kisiasa na mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo jana, Kenani Kihongosi, amesema mkutano huo pia ulipitisha Hati ya Uanzishwaji na Uendeshaji wa APPI na kuridhia uongozi wake wa kwanza wenye wajumbe 17.
Amesema uongozi huo utaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha National Democratic Congress (NDC) cha Ghana, Johnson Asiedu Nketiah, akisaidiwa na makamu wenyeviti wanaowakilisha kanda mbalimbali za Afrika, akiwamo Dkt. Migiro kwa upande wa Afrika Mashariki.
Kihongosi amesema CCM inapokea kwa heshima na shukrani dhamana hiyo ya uongozi, ambayo itatoa fursa kwa chama kuendelea kuchangia katika kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya vyama vya siasa barani Afrika.
Amesema mkutano huo pia ulipitisha Azimio la Addis Ababa, linalosisitiza wajibu wa vyama vya siasa katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, utawala bora, uwekezaji wenye tija, maendeleo ya viwanda, biashara baina ya nchi za Afrika na upatikanaji wa ajira, hususan kwa vijana.
Aidha, azimio hilo limeweka msisitizo katika mchango wa vijana na wanawake katika uongozi na maendeleo ya kiuchumi, likisisitiza umuhimu wa ushiriki wao katika michakato ya maamuzi na maendeleo ya Bara la Afrika.
Katika hatua nyingine, mkutano huo umekubaliana kuanzisha Baraza la Shule na Taasisi za Vyama vya Siasa Barani Afrika (CAPPSI) pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mageuzi (PATL), kwa lengo la kuimarisha elimu ya siasa, utafiti, maandalizi ya viongozi na uwezo wa vyama kusimamia utekelezaji wa sera za maendeleo.
Vilevile, washiriki wamekubaliana kuanza mashauriano ya kuandaa Ajenda ya APPI 2040, itakayotoa mwelekeo wa ushirikiano wa vyama vya siasa katika kutekeleza vipaumbele vya maendeleo ya Afrika, sambamba na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.
Amesema CCM itaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa barani Afrika katika kuimarisha taasisi za kisiasa, kuendeleza mshikamano wa Afrika na kuchangia utekelezaji wa ajenda za maendeleo kwa ustawi wa wananchi.