Msomi ashauri PPP inufaishe pande zote

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dkt. Lutengano Mwinuka, ameshauri kuwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) unapaswa kunufaisha pande zote mbili zinazoingia makubaliano ya kutekeleza miradi ya kimkakati.

Mhadhiri huyo ametoa maoni hayo wakati akichangia hoja katika mhadhara wa umma uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katikati ya wiki hii ukiangazia nafasi ya PPP katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 alisema kuna umuhimu kuhakikisha Serikali na sekta binafsi zote zinanufaika ili ushirikiano huo uwe na tija na uendelevu.

“Bado dhana ya win-win lazima iangaliwe, kwa maana Serikali iweze kufaidika lakini pia sekta binafsi ifaidike ili ubia huo uwe na maana,” amesema.

Ameeleza dhana ya ubia haipaswi kuangaliwa kwa mtazamo finyu wa kampuni na mashirika pekee, bali inapaswa kutafsiriwa kwa upana zaidi kwa kuhusisha wadau mbalimbali wenye uwezo wa kuchangia maendeleo.

Dkt Mwinuka amesema ni wakati wa kupanua wigo wa fikra kuhusu ubia na kutafuta njia mbadala za kushirikiana na wadau tofauti ili kuvutia mitaji na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *