Na Mwandishi Wetu
Mhadhara wa umma uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, umewakutanisha wataalamu na wanazuoni mbalimbali kujadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika kufanikisha maendeleo ya taifa.
Katika mhadhara huo, Mhadhiri wa Chuo hicho kutoka Idara ya Mafunzo ya Biashara na mtaalamu wa PPP, Dkt. Jasinta Msamula, amemuelezea Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, kuwa ni mtaalamu mwenye uzoefu mkubwa katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya ubia.

Dkt. Jasinta amesema Kafulila ana uelewa mpana wa mifumo ya PPP na mchango wake katika kuunganisha sekta ya umma na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Mhadhara huo uliobeba mada “Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kama chachu ya kufikia malengo ya Dira 2050”, uliwapa washiriki fursa ya kujadili nafasi ya PPP katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, Kafulila ameelezwa kuwa ni miongoni mwa wataalamu wanaoendelea kuhamasisha matumizi ya PPP kama nyenzo ya kupunguza mzigo wa uwekezaji kwa Serikali, huku ikiongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kufanikisha malengo ya muda mrefu ya taifa.

