Na Salha Mohamed
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, imekusanya sh. bilioni 126.6, sawa na zaidi ya asilimia 85 ya lengo la mapato kwa mwaka wa fedha unaomalizika mwezi huu, mafanikio yaliyoiwezesha kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za miundombinu, elimu na afya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa rasilimali pamoja na utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Akizungumza mbele ya Kamati hiyo, Mabelya amesema sehemu ya mapato hayo imewezesha kuendelea kwa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kwa Mpalange-Mwanagati-Kitunda yenye urefu wa kilomita 6.5, ambayo inalenga kurahisisha shughuli za biashara na uzalishaji katika maeneo ya Kwa Mpalange, Mwanagati na Kitunda.
Amesema katika sekta ya afya, ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mchikichini umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 7.4 utakapokamilika, huku kituo hicho kikitarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 325,835 kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Ilala pamoja na baadhi ya maeneo ya Kinondoni na Temeke.
Mabelya amesema mafanikio ya makusanyo hayo pia yameiwezesha halmashauri kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Bunge yanayotaka halmashauri zenye makusanyo makubwa kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa barabara za ndani ili kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Sekretarieti ya Mkoa kuhakikisha changamoto za wananchi katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uwezeshaji wa kiuchumi zinaendelea kutatuliwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema ziara ya kamati hiyo imekuwa chachu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Florent Kyombo, amesema Jiji la Dar es Salaam ni kioo cha taifa na kubainisha kuwa kamati hiyo imeipokea taarifa iliyowasilishwa.




