Na Saha Mohamed
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limefunga rasmi mashindano ya Kombe la CNS Cup 2026 katika Kambi ya JKT Mgulani jijini Dar es Salaam, likisisitiza michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha nidhamu, uzalendo, afya na kuibua vipaji vya vijana wanaojitolea kulitumikia taifa.
Akifunga mashindano hayo leo Juni 23,2026 kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amesema michezo ni sehemu muhimu ya mafunzo ya JKT kwa kuwa inawajengea vijana uwezo wa kimwili na kiakili, pamoja na kuwaimarisha katika misingi ya nidhamu, kujituma, uongozi na mshikamano unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu ya kijeshi.
Ameongeza michezo ni ajira na ni fursa ya maendeleo kwa vijana.

“Wale waliopata nafasi ya kuchaguliwa wanapaswa kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii na kulinda vipaji vyao kwa manufaa ya JKT na taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesema mashindano ya CNS Cup yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo kutoka vikosi mbalimbali vya JKT, ambao baadaye hujumuishwa katika timu teule za jeshi hilo kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kijeshi na yale ya kitaifa.
Aidha, amewahimiza washiriki ambao hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kutokata tamaa, bali kuendelea kujifua zaidi kwa kuwa bado kuna fursa nyingine za kuwakilisha JKT katika mashindano mbalimbali.
Brigedia Jenerali Mnyani alisema JKT tayari limeanza maandalizi ya mashindano ya KDF Cup na BAMATA, akibainisha kuwa lengo ni kuongeza ushindani na kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita.
Pia amewapongeza makamanda, walimu, viongozi na washiriki wote kwa kuonesha nidhamu ya hali ya juu, ushindani wa haki na uvumilivu katika kipindi chote cha mashindano hayo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha JKT Mgulani, Kanali Ernest Sambila, amesema michuano hiyo ilianzia ngazi ya vikosi kabla ya kuendelea katika kanda tano za JKT nchini, ambapo wanamichezo walishindana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu na mingineyo.
Aidha Mkurugenzi wa Elimu, Michezo, Sanaa na Utamaduni JKT, Kanali Amos Mollo, amesema mashindano hayo yamefanikisha kupatikana kwa wanamichezo wenye vipaji watakaojiunga na timu za JKT kwa ajili ya kushiriki mashindano ya majeshi na yale ya kitaifa.
Amesema zaidi ya wanamichezo 1,600 walishiriki katika hatua mbalimbali za mashindano hayo, huku mchakato wa uteuzi ukizingatia uwezo, nidhamu na utayari wa kushiriki katika timu za jeshi.
“Michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga umoja, kuimarisha afya na kuibua vipaji vya vijana, sambamba na kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya taifa,” amesema.
