Na Mwandishi Wetu, Mbeya
HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imewakaribisha wawekezaji na wadau wa sekta binafsi kushiriki katika mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa katika eneo la Ilemi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Meya wa Jiji la Mbeya Dormohamed Issa ametoa wito huo jijini humo Jumanne, Novemba 3, 2026, wakati wa ufunguzi wa kikao cha utambulisho wa mradi huo.

Kikao hicho kimewashirikisha wawakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre).
Akizungumza katika kikao hicho, Meya Issa amesema mradi huo unalenga kuchukua nafasi ya machinjio ya zamani ambayo hayakidhi viwango vinavyotakiwa.
“Mradi huo utahakikisha wananchi wanapata nyama safi na salama iliyokaguliwa kwa kina, huku ukiongeza thamani katika sekta ya mifugo na kusaidia kukuza uchumi wa wafugaji,” amesema.

Meya huyo amesema kuwa kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Halmashauri ya Jiji la Mbeya, kwa kushirikiana na Tamisemi kutafuta wawekezaji wenye uwezo, uzoefu na utayari wa kushirikiana nayo kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa manufaa na maendeleo ya wananchi.
“Halmashauri inawakaribisha wawekezaji kutumia fursa hiyo kutoa maoni, mapendekezo na ushauri kuhusu muundo wa mradi, uwezo wao wa kuwekeza, namna bora ya kugawana majukumu na mfumo endelevu wa kuendesha machinjio hayo ya kisasa,” amesema.


