Ewura yaweka wazi sababu ya bidhaa za mafuta kupanda bei

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imesema kuendelea kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, eneo ambalo Tanzania huagiza sehemu kubwa ya mafuta yake, kumeongeza gharama za usafirishaji na bima, hivyo kusababisha kupanda kwa bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

Kutokana na hali hiyo, bei za mafuta hayo zimepanda kuanzia leo, huku dizeli ikiuzwa kwa Shilingi 4,128 kwa lita katika Jiji la Dar es Salaam, ikifuatiwa na mafuta ya taa kwa Shilingi 4,117 na petroli Shilingi 4,083 kwa lita.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa leo na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Salum Mnuna, inaonesha kuwa ongezeko hilo limejitokeza katika bandari zote tatu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Katika Bandari ya Dar es Salaam, petroli imepanda kutoka Shilingi 4,057 za Oktoba hadi Shilingi 4,083 kwa lita, sawa na ongezeko la Shilingi 26.

Dizeli imepanda kutoka Shilingi 4,086 hadi Shilingi 4,128 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 42, huku mafuta ya taa yakiongezeka kutoka Shilingi 4,067 hadi Shilingi 4,117, sawa na Shilingi 50 kwa lita.

Katika Bandari ya Tanga, petroli imepanda kutoka Shilingi 4,123 hadi Shilingi 4,149 kwa lita, huku dizeli ikiongezeka kutoka Shilingi 4,152 hadi Shilingi 4,194. Mafuta ya taa yamepanda kutoka Shilingi 4,133 hadi Shilingi 4,183 kwa lita.

Kwa upande wa Bandari ya Mtwara, petroli imepanda kutoka Shilingi 4,170 hadi Shilingi 4,183 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 13, huku dizeli ikipanda kutoka Shilingi 4,199 hadi Shilingi 4,231, sawa na ongezeko la Shilingi 32.

Mafuta ya taa katika bandari hiyo yameongezeka kutoka Shilingi 4,180 hadi Shilingi 4,220 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 40.

Hata hivyo, ongezeko hilo limekuja wakati bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia zikishuka kidogo Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na Septemba.

Katika kukabiliana na athari za mabadiliko hayo, Serikali imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia na kuchukua hatua kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta pamoja na kupunguza makali ya bei kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuwa huru kuuza bidhaa hizo kwa bei za ushindani, lakini zisizidi bei kikomo zilizowekwa wala kuwa chini ya viwango vinavyoruhusiwa.

Bei hizo zimekokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za mwaka 2022, zilizotangazwa Januari 28, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 57, pamoja na marekebisho yaliyotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 761A la Oktoba 30, 2023 na mabadiliko ya Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja za mwaka 2024.

Ewura pia ilivitaka vituo vyote vya mafuta kuweka mabango yanayoonekana vizuri yanayoonyesha bei za bidhaa hizo, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa.

“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani,” imeeleza taarifa hiyo.

Mamlaka hiyo ilionya kuwa kuuza mafuta bila kuweka mabango yanayoonyesha bei kwa uwazi ni kosa, na kituo kitakachokiuka matakwa hayo kitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni husika.

Aidha, Ewura imewataka wauzaji wa mafuta kutoa stakabadhi za mauzo kupitia mashine za Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), huku wanunuzi wakitakiwa kuhakikisha wanapokea stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo zinapaswa kuonyesha jina la kituo, tarehe ya ununuzi, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Kwa mujibu wa Ewura, stakabadhi hizo zitakuwa ushahidi kwa wanunuzi endapo kutatokea malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei inayozidi kikomo au bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Pia, zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zinazotokana na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *