DIB: Hauhitaji kulipia Bima kulinda fedha zako benki

Na Salha Mohamed

BODI ya Bima ya Amana (DIB), imesema wananchi wanaoweka fedha katika benki na taasisi za fedha nchini hawalipii gharama yoyote ya bima ya amana, badala yake benki ndizo zinazochangia ili kulinda fedha za wateja wao endapo taasisi hizo zitafungwa au kuwekwa chini ya ufilisi.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mwandamizi wa Bodi hiyo, Joyce Shala, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Shala amesema DIB ni taasisi ya Serikali iliyopewa dhamana ya kulinda amana za wananchi katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

2-2-1024x768 DIB: Hauhitaji kulipia Bima kulinda fedha zako benki

“Bima ya amana ni tofauti na bima nyingine. Mwananchi hachangii chochote. Kwa mujibu wa sheria, benki zote zenye leseni ndizo zinazochangia kwa niaba ya wateja wao ili kuhakikisha fedha zao zinalindwa,” amesema Shala.

Amesema mfumo huo umewezesha asilimia 99 ya waweka amana nchini kulipwa fidia kwa asilimia 100 endapo benki itafungwa au kuwekwa chini ya ufilisi.

“Tunawalipa fidia kuanzia shilingi moja hadi shilingi milioni 7.5. Asilimia 99 ya wateja wa benki hupata fedha zao zote, kwa wale wenye fedha zinazozidi kiwango hicho, tunasimamia ufilisi wa benki husika kwa kukusanya mali na madeni ili waweze kulipwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amefafanua kuwa DIB hukusanya michango kutoka benki na taasisi za fedha, huiwekeza ili kuimarisha mfuko wa fidia na kuhakikisha wananchi wanalipwa kwa wakati pale inapohitajika.

3-2-1024x768 DIB: Hauhitaji kulipia Bima kulinda fedha zako benki

Aidha, amesema tangu mwaka 2025 bodi hiyo imeongezewa jukumu la kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kupunguza hasara katika benki zinazokabiliwa na changamoto za kiuendeshaji ili kulinda maslahi ya wateja na kuhakikisha huduma za kibenki zinaendelea bila usumbufu.

Shala amesema DIB inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia Maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Huduma za Fedha na programu mbalimbali za uhamasishaji katika kanda zote nchini.

“Tunataka wananchi wote wawe na uelewa kwamba fedha wanazoweka benki zinalindwa kwa mujibu wa sheria. Karibuni katika banda letu kupata elimu hii bila malipo,” amesema.

4-2-1024x768 DIB: Hauhitaji kulipia Bima kulinda fedha zako benki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *