DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 hakuna mwanafunzi atakayejiunga Kidato cha Kwanza bila kuwa na darasa, kiti na meza, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.

Mpogolo ameyasema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima, iliyolenga kutembelea vituo vya malezi na makuzi ya watoto.

1003767496-1024x682 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Amesema katika maandalizi ya mfumo mpya wa elimu ya msingi hadi Kidato cha Nne, Halmashauri hiyo imejipanga kuhakikisha kila mtoto anayestahili kuanza masomo anapata nafasi na mazingira bora ya kujifunzia.

Ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga zaidi ya Sh bilioni 12 kwa ajili ya elimu ya msingi na Sh bilioni 19 kwa elimu ya sekondari.

1003767477-1024x682 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Amesema fedha hizo ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi linalotokana na mfumo wa udahili wa wanafunzi wengi (Double Cohort), kuongeza uwezo wa miundombinu ya shule na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa fursa ya kupata elimu.

Katika hatua nyingine, Mpogolo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu kupitia mpango wa elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi Kidato cha Sita.

1003767495-1024x682 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Amesema uwekezaji huo umechangia kupunguza mzigo wa gharama za elimu kwa wazazi na walezi.

Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kila mtoto kupata haki ya elimu na fursa ya kufikia ndoto zake, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu kupitia mikopo ya elimu ya juu.

1003767486-1024x682 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Akizungumzia masuala ya malezi na makuzi ya watoto, Mpogolo amempongeza Waziri Gwajima kwa kuanzisha programu ya kutembelea vituo vya malezi na makuzi ya watoto, akisema itasaidia kubaini changamoto zinazowakabili watoto, hususan wanaolelewa na mabibi zao kutokana na changamoto za kifamilia zinazowakumba wazazi wao.

Amesema pamoja na upendo mkubwa walionao mabibi kwa wajukuu zao, malezi bora yanahitaji pia ujuzi, mazingira salama na mifumo inayozingatia ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili, kihisia na kijamii.

1003767487-1024x682 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

“Mheshimiwa Waziri, tunaona ziara yako inaenda kutibu kidonda hiki. Tunahitaji kuhakikisha watoto wetu wanapata malezi bora yanayozingatia mahitaji yao ya ukuaji na makuzi.

Tunakushukuru sana kwa programu hii na tunaomba uendelee kuifikisha katika maeneo na vituo vyote vinavyohusika na malezi ya watoto,” amesema.

1003767488-1024x576 DC Mpogolo: Hakuna mwanafunzi atakayekosa darasa, kiti 2028

Mpogolo ameshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika elimu na ustawi wa watoto, huku akimpongeza Waziri Gwajima kwa juhudi za kuimarisha mifumo ya malezi na makuzi, akisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa yanahitaji watoto wanaopata elimu bora, malezi bora, maadili na mazingira salama ya kukua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *