Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo

WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.25.37-1-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) leo imezindua rasmi Tawi lake jipya la Ubungo lililopo katika jengo la EACLC, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyekuwa Mgeni Rasmi, amesema sekta ya benki ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo, wajasiriamali, mama lishe na machinga.

“Sekta ya benki ni mhimili muhimu katika maendeleo ya nchi. Inachochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama viwanda, kilimo, uvuvi, ujenzi na biashara. Kupitia mikopo na huduma za kifedha, wananchi wanawezeshwa kupanua shughuli zao na kuongeza kipato,” amesema Chalamila.

Aidha, ameipongeza TCB kwa kuoanisha mikakati yake na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, hususan katika kuimarisha biashara ndogo na za kati (SMEs), ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji wa jamii.

Ameongeza kuwa, uwekezaji wa tawi hilo ubungo ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya kifedha na kukuza shughuli za kiuchumi katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za biashara na usafirishaji.

Chalamila pia ametoa wito kwa taasisi za kifedha kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji kama viwanda na kilimo, pamoja na kuangalia namna ya kupunguza viwango vya riba ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na mikopo.

Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama wa kifedha hususan dhidi ya uhalifu wa kimtandao.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo, amesema uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kupanua huduma zake na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kifedha kwa urahisi.

“Amesema hadi sasa TCB ina jumla ya matawi 82 nchini kote na zaidi ya mawakala 7,000, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na matawi 20.

Benki ya TCB imeendelea kukua na kuimarika kifedha pamoja na kupanua huduma zake ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Hadi kufikia Machi 2026, Mali za benki zimefikia takribani Sh. trilioni 2.4, huku amana za wateja zikifikia Sh. trilioni 1.7 na mikopo kwa wateja kufikia zaidi ya Sh. trilioni 1.5.”

“Tunajivunia mafanikio haya ambayo yanaonesha imani kubwa ya wananchi kwa benki yetu na mchango wetu katika kukuza uchumi wa taifa. Tutaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wananchi wa kipato cha chini, wajasiriamali wadogo na wa kati, pamoja na vijana na wanawake,” amesema Mihayo.

Ameongeza kuwa benki imeendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, huku idadi ya watumiaji wa huduma hizo ikiendelea kuongezeka kwa kasi. Pia, kupitia huduma za Trade Finance, TCB iko tayari kusaidia wafanyabiashara wanaojihusisha na uagizaji na usafirishaji wa bidhaa kupanua biashara zao.

Mihayo amesisitiza kuwa ufunguzi wa tawi hilo ni uthibitisho wa dhamira ya TCB katika kuendeleza ujumuishi wa kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Ameongeza kuwa benki imeendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali ili kuchochea maendeleo ya biashara na ajira. Sambamba na uzinduzi wa tawi hili kwa Mkoa wa Dar es kuna matawi mengine manne tunayotarajia kuzindua katika mkoa huu ikiweno Tegeta, Msaki, Kariakoo Sokoni na Kariakoo DDC.

“Aidha, tunampango wa kuongeza matawi mengine mawili kwenye mkoa huu, ikiwamo Goba na Mbezi.

Kwa wakazi wa Ubungo na maeneo jirani, TCB imetoa wito kwao kutumia huduma zake mbalimbali ikiwemo kufungua akaunti, kupata mikopo ya kukuza biashara na kutumia huduma za kidijitali kwa urahisi na usalama. Uzinduzi wa Tawi la TCB Ubungo unatarajiwa kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi katika eneo hilo na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za Serikali za kujenga uchumi jumuishi na shindani.

WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.26.05-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.25.58-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.25.37-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.24.06-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.23.58-1024x683 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.23.50-683x1024 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.23.39-683x1024 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo
WhatsApp-Image-2026-04-24-at-08.23.33-683x1024 Benki ya TCB yazindua tawi jipya Ubungo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *