TMDA yapiga marufuku Dawa ya Mifugo ya Hi-tet 120

IMG_20240707_120036_323-1024x669 TMDA yapiga marufuku Dawa ya Mifugo ya Hi-tet 120

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepiga marufuku rasmi utengenezaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa ya mifugo inayojulikana kwa jina la kibiashara Hi-tet 120.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kuwa baadhi ya wasambazaji na wauzaji wasio waaminifu walikuwa wakijihusisha na udanganyifu wa kubadilisha lebo na kufungasha upya dawa hiyo na kisha kuzirudisha sokoni kwa lengo la kujipatia faida isivyo halali.

Akizungumza kuhusu marufuku hiyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo, Mei 21, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema dawa ya Hi-tet 120 ina kiambata hai kinachoitwa kitaalamu Oxytetracycline Hydrochloride na imekuwa ikipatikana sokoni kwa bei ya juu zaidi ikilinganishwa na dawa nyingine zenye kiambata sawa.

Amesema uchunguzi wa TMDA umeonyesha kuwa dawa hii imekuwa ikighushiwa mara kwa mara kutokana na urahisi wa kifungashio chake, ambacho ni chupa ya kahawia na boksi la njano.

“Hali hii imekuwa ikitoa mwanya kwa wauzaji wasio waaminifu kufanya udanganyifu na hivyo kuhatarisha afya ya mifugo na jamii kwa ujumla.

“Kutokana na changamoto ya kughushiwa mara kwa mara, TMDA imepiga marufuku utengenezaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa hii kuanzia tarehe ya tangazo hili. Mtu au kampuni yeyote itakayobainika kuendelea na biashara ya dawa hii itachukuliwa hatua za kisheria,” amesisitiza Dkt. Fimbo.

Screenshot-2026-05-21-150903 TMDA yapiga marufuku Dawa ya Mifugo ya Hi-tet 120

Aidha, TMDA imetoa wito kwa wananchi kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa bandia, duni na ambazo hazijasajiliwa kwa kutoa taarifa za watu au kampuni zinazojihusisha na biashara haramu ya dawa.

Wananchi wanahimizwa kutoa taarifa katika vituo vya Polisi vilivyo karibu, ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Ruvuma, Tabora na Geita, au kupitia barua pepe info@tmda.go.tz na simu ya bure 0800110084.

Marufuku hii inalenga kulinda afya ya mifugo na jamii kwa ujumla dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na dawa bandia na zisizokidhi viwango.

TMDA imeendelea kusisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na wadau wote ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa dawa na kuimarisha mapambano dhidi ya udanganyifu wa dawa nchini.

Kwa hatua hii, TMDA imeonesha dhamira ya dhati ya kulinda afya ya jamii na mifugo, huku ikitoa tahadhari kwa wasambazaji na wauzaji wote kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *