
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema imebaini uwapo wa dawa ya binadamu ya vidonge ya kuongeza nguvu za kiume ambayo haijasajiliwa yenye jina la kibiashara lijulikanalo kama VEGA – 100 Tablets.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, imeeleza kuwa, uchunguzi wa kina wa TMDA umebaini kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio
waaminifu wanaojihusisha na usambazaji na uuzaji wa dawa hiyo kwenye maeneo
mbalimbali nchini.
“TMDA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura, 219 yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Katika utekelezaji wa majukumu yetu tumeini uwapo wa dawa hii ambayo haijasajiliwa nchini,” ameeleza Dkt. Fimbo katika taarifa hiyo na kufafanua zaidi kuwa;
“Dawa yenye jina husika kama inavyoonekana kwenye picha hapa chini ina kiambata hai
(active ingredient) chenye jina la kitaalam Sildenafil Citrate na kwenye lebo zake jina la
mtengenezaji linaloonekana ni Signature Pharmaceuticals Ltd, India.”

Ameeleza zaidi kuwa dawa hii hutumika kwa ajili ya kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume wenye tatizo la kutosimamisha uume wakati wa tendo la ndoa.
“Matumizi holela ya dawa hii ni hatari kwa afya ya binadamu na inaweza kusababisha
madhara makubwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushusha presha au shinikizo la chini la damu, uume kubaki umesimama kwa muda mrefu hadi hata kuzidi masaa manne, kupoteza uwezo wa kuona kunakoweza kutokea kwa ghafla na kupoteza uwezo wa kusikia ikiambatana na kusikia sauti kwenye masikio,” amesema.
Dkt. Fimbo anasema madhara mengine madogo ni pamoja na kuumwa kichwa, kuona maruerue, pua kujaa makamasi, kupata kiungulia, kushindwa kumeng’enya chakula vizuri, kutoona vizuri na maumivu ya misuli au mgongo.
“Mamlaka inapenda kuutahadharisha umma kuwa dawa tajwa haifai kwa matumizi ya
binadamu, na kwamba ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa kwa kuwa haijasajiliwa na TMDA,” amesema Dkt. Fimbo.
Aidha, TMDA inatoa wito kwa wananchi wote kutoa taarifa za kampuni au watu wanaojihusisha
na usambazaji wa dawa hii ili hatua za kuiondoa kwenye soko ziweze kuchukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahusika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Amewataka wananchi kutoa taarifa zinaweza kutolewa kwenye kituo chochote cha Polisi kilicho karibu au
kuwasilishwa katika Ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Ruvuma, Tabora, na Geita, au kupitia barua pepe: info@tmda.go.tz, au kupiga simu ya bila malipo Na. 0800110084.
“Wananchi pia wanaaswa kutotumia dawa bila kupata ushauri wa madaktari, wafamasia au wataalam wengine wa afya kwa kuwa dawa ni kemikali zenye sumu na zinaweza kusababisha madhara ikiwa ni pamoja na vifo.
“Tushirikiane kwa pamoja katika mapambano dhidi ya dawa bandia, duni na ambazo hazijasajiliwa ili kulinda afya zetu sote,” amesema Dkt. Fimbo.