TBA yatwaa Tuzo Sabasaba, yajipanga kuwa bora Afrika

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umesema tuzo ya mshindi wa pili katika kipengele cha milki iliyopatikana kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ni mwanzo wa safari ya mafanikio makubwa, huku ukieleza kuwa unajipanga kwenda viwango vya juu zaidi vya kimataifa.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, amesema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kufanikisha lengo la kuwapa Watanzania taarifa muhimu kuhusu kazi zinazofanywa na TBA.

“Safari ya TBA katikati ya Maonesho ya 50 ya Biashara Sabasaba imekuwa yenye mafanikio makubwa sana. Kama unavyofahamu TBA tunasema hatuna jambo dogo kwetu, kila kitu tunakichukulia serious sana,” amesema Lumuli.

2-23 TBA yatwaa Tuzo Sabasaba, yajipanga kuwa bora Afrika

Amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo, TBA ilikusudia kuwahudumia Watanzania kwa kuwapa taarifa kuhusu majukumu yake kama wakala wa Serikali, ikiwemo kutoa huduma za ushauri, ujenzi na kusimamia milki za Serikali.

“Tulikuwa tunakusudia kuwahudumia Watanzania kwa kuwapa taarifa muhimu ya kazi ambazo tunazifanya. Kama tulivyo wakala wa Serikali tunatoa huduma za ushauri, za ujenzi, lakini sisi tunasimamia milki za Serikali ambayo ndiyo kazi yetu kubwa,” amesema.

Lumuli amesema kupitia banda la TBA, wananchi waliweza kuona kazi inayofanywa na Serikali kupitia taasisi hiyo, ubora wa majengo yanayojengwa pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana.

Amesema TBA pia imewatambulisha Watanzania fursa za kuwekeza katika milki za Serikali kwa kushirikiana na wakala huo ili waweze kunufaika na huduma hizo.

“Watanzania pia wameweza kuona fursa ambazo TBA tunazo za uwekezaji ili Watanzania waweze kufaidika na huduma zetu na milki za Serikali katika uwekezaji na kufaidika na hizo huduma ni kushirikiana na TBA ili tuweze kuwekeza katika milki zilizopo nchi nzima,” amesema.

3-20 TBA yatwaa Tuzo Sabasaba, yajipanga kuwa bora Afrika

Lumuli amesema kwa sasa TBA ina milki mbalimbali 149 zilizoainishwa, huku 38 zikiwa tayari zimetangazwa kwa ajili ya uwekezaji.

“Kwa sasa tunamilki mbalimbali ambazo tumeziainisha 149, lakini tumetangaza 38 ambazo tunategemea kila Mtanzania ambaye ana nia njema ya kuwekeza kwenye real estate ana uwezo wa kuja kwetu na kuweza kuwekeza,” amesema.

Amesema wananchi waliotembelea banda la TBA wamejionea namna taasisi hiyo ilivyojipanga kutoa huduma bora za usimamizi wa milki, jambo lililochangia kupata tuzo hiyo.

“Leo tumeweza kushinda tuzo hii kwa kuwa washindi wa pili kwenye kipengele cha milki na tuzo hii kwetu ni mwanzo wa safari yetu ya ushindi,” amesema.

Lumuli amesema TBA tayari imeanza kutekeleza mkakati mpya wa mwaka 2026/27 hadi 2031 wenye lengo la kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma bora zaidi.

“TBA tumejipanga kwenda Afrika. Tumeanza kutekeleza mkakati mpya ambao umeanza 2026/27 utakaoisha 2031, lakini sisi dira yetu ni kwenda Afrika na kutoa huduma bora za makazi, ushauri pamoja na ujenzi. Si tu, lakini tuwe bora Afrika nzima,” amesema.

Amesema tuzo hiyo imekuwa chachu kwa TBA kuongeza juhudi za kufikia viwango vya juu zaidi vya kimataifa katika utoaji wa huduma zake.

“Hii tuzo imetupa chachu ya kujiona tunakwenda viwango vya juu zaidi vya kimataifa,” amesema.

4-9-768x1024 TBA yatwaa Tuzo Sabasaba, yajipanga kuwa bora Afrika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *