Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema elimu ya ufundi stadi ndiyo nguzo muhimu ya kutatua tatizo la ajira na kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara nchini, huku ikiwataka Watanzania kuipa kipaumbele ili kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Uhusiano kwa umma na Masoko wa VETA, Sitta Peter, wakati akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo VETA iliibuka mshindi wa tatu katika kundi la taasisi za elimu ya juu, uendelezaji ujuzi na utafiti.
Sitta alisema ushindi huo ni ishara ya kutambuliwa kwa mchango wa VETA katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi, kufanya ubunifu unaolenga kutatua changamoto za jamii na kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
“Tunawashukuru Watanzania wote waliotembelea banda letu. Ilikuwa fursa muhimu ya kuwaonesha huduma zetu, mafunzo tunayotoa pamoja na ubunifu mbalimbali unaotokana na tafiti zinazolenga kutatua changamoto za jamii,” alisema.
Alieleza kuwa tafiti zinazofanywa na VETA hazibaki kwenye maandiko bali hubadilishwa kuwa teknolojia, bidhaa na suluhisho zinazotumika moja kwa moja na wananchi katika shughuli za kila siku.
Alifafanua kuwa wageni waliotembelea banda la VETA walijionea ubunifu wa teknolojia mbalimbali pamoja na shughuli za uzalishaji zinazofanywa na vyuo vya VETA, ambazo zimekuwa zikichangia kuongeza mapato ya taasisi na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.
“Tunafanya tafiti zinazolenga matumizi halisi ya jamii. Changamoto zinazopo kwenye jamii ndizo zinazotuongoza kubuni teknolojia na bidhaa zinazotoa suluhisho,” alisema.

Sitta alisisitiza kuwa elimu ya ufundi stadi ni mkombozi wa vijana kwa kuwa inawapa ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa, jambo linalochangia kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
“Elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni suluhisho la ajira, lakini pia ndiyo nguzo muhimu ya kusukuma uchumi wa nchi. Tunawaomba wananchi wayape kipaumbele mafunzo haya,” alisema.
Akizungumzia ushindi walioupata katika maonesho hayo, alisema ni motisha kwa VETA kuendelea kuboresha mafunzo, kuongeza ubunifu na kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Alisema tathmini iliyofanywa na waandaaji wa maonesho imeonesha kuwa huduma zinazotolewa na VETA zinaendana na mahitaji ya jamii, jambo lililowezesha taasisi hiyo kupata nafasi ya tatu.
“Kwetu huu ni msukumo wa kufanya vizuri zaidi kwa kuboresha mafunzo yetu, ubunifu wetu na bidhaa zetu ili ziendelee kuwa na manufaa kwa wananchi,” alisema.
Aidha, Sitta alisema VETA ina mchango mkubwa katika ukuaji wa biashara kwa kuwa ndiyo inayozalisha nguvu kazi yenye ujuzi inayohitajika katika viwanda, biashara na sekta nyingine za uzalishaji.
Alieleza kuwa wahitimu wengi wa VETA huanzisha miradi na biashara zao wenyewe baada ya kuhitimu, hatua ambayo huchangia kuongeza ajira, uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa.
“Biashara nyingi haziwezi kukua bila kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi. VETA ndiyo inayozalisha wataalamu hao, na wengi wa wahitimu wetu pia huanzisha biashara zao, hivyo kuchangia moja kwa moja ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema.