COASCO: Ushirika waendelea kuimarisha uchumi wa Taifa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

SHIRIKA la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limesema sekta ya ushirika imeendelea kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania, huku mazao yanayouzwa kupitia vyama vya ushirika yakiliingizia taifa zaidi ya dola za Marekani bilioni mbili kila mwaka.

Aidha, shirika hilo limesema juhudi za kuimarisha uwajibikaji na utawala bora zimeongeza idadi ya vyama vya ushirika vinavyopata hati safi za ukaguzi kutoka asilimia nne miaka iliyopita hadi zaidi ya asilimia 60 kwa sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COASCO, CPA Jeremiah Mgeta, alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Mgeta amesema sekta ya kilimo inaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa taifa kwa kuchangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa, huku ushirika ukiwa chombo muhimu cha kuwaunganisha wakulima, kuongeza thamani ya mazao na kupanua masoko.

“Kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu, lakini pia ushirika kupitia mazao yake unachangia zaidi ya dola bilioni mbili kwa mwaka. Huu ni mchango mkubwa unaostahili kuendelezwa,” amesema.

Amesema wananchi wanaotembelea banda la Wizara ya Kilimo wanapata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo nafasi ya vyama vya ushirika katika kuinua kipato cha wakulima.

Akizungumzia majukumu ya COASCO, amesema taasisi hiyo itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kutoa elimu kwa viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika pamoja na kusimamia uzingatiaji wa sheria na kanuni za uendeshaji wa vyama hivyo.

2-17 COASCO: Ushirika waendelea kuimarisha uchumi wa Taifa

“Sisi ni jicho la Serikali katika kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji. Lengo letu si kubaini kasoro pekee, bali pia kutoa ushauri utakaovifanya vyama kuwa imara zaidi,” amesema.

Amesema mafanikio ya ukaguzi yanaonekana kupitia ongezeko la vyama vinavyopata hati safi, hali inayoonyesha kuimarika kwa usimamizi wa fedha na utawala bora ndani ya vyama vya ushirika.

CPA Mgeta amesema COASCO itaanza awamu ya kwanza ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2026/27 kuanzia Julai 20 na kuwataka viongozi wa vyama kuandaa na kuwasilisha taarifa zao za fedha kwa wakati ili ukaguzi ufanyike kwa ufanisi.


Pia alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kutoa elimu na ushauri utakaosaidia kuongeza uwazi, tija na imani ya wanachama kwa vyama vyao.


Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa mazingira wezeshi yanayochochea ukuaji wa sekta ya ushirika, na kuahidi COASCO itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu ili kuongeza mchango wa ushirika katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *