Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema kuanza kwa uzalishaji kutoka kwenye visima vipya vya gesi kutasaidia kuongeza kiwango cha gesi kinachoingia kwenye bomba kuu la taifa, hatua itakayoongeza upatikanaji wa gesi kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani, magari yanayotumia gesi pamoja na matumizi ya majumbani.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mjiolojia wa TPDC, Magambo Samweli, amesema shirika hilo linatarajia kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kupitia mradi wa uchorongaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay, ambapo visima viwili tayari vimekamilika na kimoja kinaendelea kuchorongwa.
Amesema visima hivyo vinachimbwa kwa ubia kati ya TPDC na kampuni ya Maurel & Prom (M&P) kwa lengo la kuongeza kiwango cha gesi kinachozalishwa katika kitalu hicho.
Kwa mujibu wa Samweli, kati ya visima vitatu vinavyochimbwa, viwili vinalenga kuongeza uzalishaji wa gesi huku kisima kimoja kikitumika kutafuta maeneo mapya yenye akiba ya gesi asilia.
Amesema kisima kimoja kina uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 40 za gesi kwa siku, huku kingine kikitarajiwa kuzalisha futi za ujazo milioni 60 kwa siku.

Aidha, amesema TPDC kwa kushirikiana na kampuni ya ARA Petroleum inaendelea kuendeleza Kitalu cha Ruvuma, ambako tayari kumekuwa na ugunduzi mkubwa wa gesi katika eneo la Ntorya.
Samweli amesema kwa sasa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka visimani hadi Kituo cha Kuchakata Gesi cha Madimba unaendelea.
Amesema bomba hilo lenye urefu wa kilomita 34.2 na kipenyo cha inchi 14 litasafirisha gesi kutoka vitalu vya Ntorya na Ruvuma kwenda Madimba kwa ajili ya kusafishwa kabla ya kuingizwa kwenye bomba kuu la taifa linalopeleka gesi hadi Dar es Salaam.
Amesema ujenzi wa bomba hilo unatarajiwa kukamilika kati ya Novemba na Desemba mwaka huu, huku usafirishaji wa gesi kupitia bomba hilo ukitarajiwa kuanza Desemba 2026.
Amesema TPDC itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kuharakisha utafutaji na maendeleo ya rasilimali za gesi asilia ili kuhakikisha nchi inanufaika zaidi na nishati hiyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya viwanda.
