Dkt. Shimo: Matokeo ya uchunguzi wa Maabara zetu yanatambulika Kimataifa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema maabara zake zote zimepata ithibati ya kimataifa, hatua inayohakikisha matokeo ya uchunguzi yanayotolewa yanatambulika na kukubalika katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira wa GCLA, Dkt. Shimo Peter Shimo, amesema ithibati hiyo inaongeza imani kwa wananchi na wadau wanaotumia huduma za mamlaka hiyo.

Amesema GCLA ndiyo maabara ya rufaa nchini inayofanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali, zikiwemo zinazohusiana na makosa ya jinai, ubora na usalama wa bidhaa pamoja na uchafuzi wa mazingira kwa lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira.

Aidha, amesema mamlaka hiyo imepewa jukumu la kusimamia maabara zote za kemikali nchini ili kuhakikisha zinatoa matokeo yenye ubora yanayokubalika kitaifa na kimataifa.

2-11-1024x830 Dkt. Shimo: Matokeo ya uchunguzi wa Maabara zetu yanatambulika Kimataifa

Dkt. Shimo amesema GCLA pia inasimamia matumizi salama ya kemikali za viwandani na majumbani kwa mujibu wa Sheria Na. 3 ya mwaka 2003, pamoja na kusimamia sheria zinazohusu vinasaba vya binadamu na kuhakikisha maabara zote zinazofanya uchunguzi wa kemikali nchini zinazingatia viwango vinavyotakiwa.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo imepanua huduma zake katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kaskazini (Arusha), Kati (Dodoma), Kusini (Mtwara na Songea), Ziwa (Mwanza na Geita) pamoja na Kanda ya Mashariki (Tanga) ili kuwafikishia wananchi huduma kwa ukaribu zaidi.

Katika Maonesho ya Sabasaba, amesema wataalamu wa GCLA wanatoa elimu kuhusu namna ya kuwasilisha sampuli kwa uchunguzi, matumizi salama ya kemikali, taratibu za usajili kwa wanaojihusisha na kemikali pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Amewahimiza wananchi kutembelea banda la GCLA katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu huduma za maabara, matumizi salama ya kemikali na uchunguzi wa sampuli mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *