Tanzania yalenga kuzalisha umeme wa Nyuklia

IMG-20260705-WA0042-1 Tanzania yalenga kuzalisha umeme wa Nyuklia

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imesema Serikali inalenga ndani ya kipindi cha takribani miaka saba kufikia hatua ya kuzalisha umeme wa nyuklia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya uchumi na viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, alisema Tanzania kwa sasa ipo katika hatua za maandalizi kabla ya kuingia rasmi kwenye awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo unaoongozwa na miongozo ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Alisema katika awamu ya kwanza Serikali inalenga kuandaa mfumo imara wa kisheria, sera na taasisi zitakazosimamia matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia ili kuhakikisha hakuna madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi wala mazingira.

“Tunataka kuhakikisha msingi wa matumizi ya nishati ya nyuklia unakuwa salama na wenye kuzingatia viwango vyote vya kimataifa kabla ya kuanza uzalishaji wa umeme,” alisema Prof. Najat.

Aliongeza kuwa tayari TAEC imewaalika wataalamu wa kimataifa kufanya tathmini ya kiwango cha utayari wa Tanzania kuingia katika mpango huo. Alisema endapo tathmini hiyo itaridhisha, nchi itapata kibali cha kuendelea na hatua inayofuata ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Prof. Najat, Serikali inalenga ndani ya kipindi cha takribani miaka saba kufikia hatua ya kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa nyuklia, hatua ambayo itasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya maendeleo ya uchumi na viwanda.

Akizungumzia upatikanaji wa malighafi, alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na akiba ya madini ya urani, ambayo ndiyo malighafi muhimu katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia. Hata hivyo, alifafanua kuwa urani haiwezi kutumika moja kwa moja bila kupitia mchakato maalumu wa kiteknolojia unaohitaji uwekezaji mkubwa na teknolojia ya hali ya juu.

Alisema katika hatua za awali, urani itachimbwa nchini kabla ya kusafirishwa katika nchi zenye uwezo wa kuichakata, ikiwemo Urusi, ili kuzalishwa mafuta ya nyuklia ambayo baadaye yatarejeshwa nchini kwa matumizi ya kuzalisha umeme.

Aidha, Prof. Najat alisema mradi wa kwanza wa uchimbaji wa urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju mkoani Ruvuma, huku tafiti zikiendelea katika maeneo mengine nchini kubaini uwepo wa akiba zaidi ya madini hayo kwa ajili ya uchimbaji wa kibiashara.

Aliwahimiza wananchi kuwa na uelewa sahihi kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuondoa hofu isiyo na msingi, akisisitiza kuwa hatua zote zinazochukuliwa zinafuata viwango vya kimataifa vya usalama na zinalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika na nishati hiyo kwa maendeleo ya Taifa bila kuhatarisha afya za wananchi wala mazingira.

IMG-20260705-WA0041-1 Tanzania yalenga kuzalisha umeme wa Nyuklia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *