Na Salha Mohamed
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, amekipongeza Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kwa kuendelea kutoa fursa za mafunzo na ujuzi kwa watu wenye mahitaji maalumu, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji na uchumi.
Mbali na pongezi hizo, Balozi Salum ameahidi kuwatafutia mitaji mafundi wawili wa kushona nguo wenye ulemavu wa mikono aliokutana nao katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ili kuwawezesha kupanua shughuli zao na kujitegemea zaidi kiuchumi.
Kauli hiyo aliitoa alipotembelea Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kukagua hatua za mwisho za maandalizi ya maonesho hayo, ambapo pia alijionea bidhaa na huduma mbalimbali zinazotarajiwa kuoneshwa.

Aidha, aliwapongeza waandaaji wa maonesho pamoja na washiriki kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki mwaka huu, akibainisha kuwa mahitaji ya nafasi za maonesho yalikuwa makubwa kutokana na hamasa iliyoonekana.
Katibu Mkuu huyo alisema Serikali ina matarajio makubwa kwamba maonesho ya mwaka huu yatakuwa miongoni mwa yaliyofanikiwa zaidi kwa kuvutia washiriki wengi, kuongeza fursa za biashara na kuleta manufaa kwa wananchi.
Akizungumzia bidhaa za wazalishaji wa ndani, Balozi Salum alisema ameridhishwa na ubora wake, hususan zinazozalishwa na wajasiriamali wanawake ambao wameendelea kuboresha vifungashio pamoja na kuzingatia viwango vinavyohitajika katika ushindani wa soko la ndani na kimataifa.
Wakizungunza kwa nyakati tofauti wananchi walioshiriki katikati maonesho hayo walisema “Maonesho ya mwaka huu yamekuwa mazuri sana. Tumepata nafasi ya kuona bidhaa nyingi zinazozalishwa hapa nchini na kupata elimu na kujionesa ubunifu kutoka VETA, Ninaamini Sabasaba imeendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wananchi na watoa huduma,” Asha Mwinuka, Mkazi wa Dar es Salaam.

Aidha Hamisi Juma, Mfanyabiashara kutoka Morogoro alisema maonesho hayo yamemsaidia kupata masoko mapya na kujifunza namna ya kuboresha biashara yake.
“Nimefurahishwa na ushiriki mkubwa wa taasisi za Serikali na sekta binafsi ambazo zinatoa elimu na huduma moja kwa moja kwa wananchi. Ni matarajio yangu kwamba maonesho yataendelea kuwa makubwa zaidi na kuwavutia washiriki wengi zaidi ndani na nje ya nchi,”alisema.
Alisema VETA imekua kiungo muhimu katikati kuwakomboa watu wenye mahitaji maalumu katikati kuvumbua na kujifunza mambo mbali mbali yanayowasaidia katikati maisha Yao ya kila siku.

