
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
MAFUNZO ya ufundi stadi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yameendelea kuzaa matunda, huku wahitimu wake wakitumia ujuzi walioupata kubuni teknolojia zinazoongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo nchini.Mmoja wa wahitimu hao, Ernest Maranya, amesema baada ya kuhitimu mafunzo ya VETA alianzisha kampuni yenye makao makuu jijini Dar es Salaam inayobuni na kutengeneza mashine za kusindika mazao mbalimbali ikiwemo karanga, kahawa na karafuu.Amesema mashine hizo zimekuwa zikiwasaidia wakulima na wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuyapeleka sokoni, hatua inayochangia kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza mapato.Maranya amesema huduma za kampuni yake tayari zimewafikia wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, ambapo baadhi yao wamefanikiwa kuanzisha au kupanua shughuli za uzalishaji kwa kutumia mashine hizo.Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ujuzi wa vitendo alioupata VETA, ambao umemwezesha kujiajiri na kutoa ajira pamoja na suluhisho kwa sekta ya kilimo kupitia teknolojia za ndani.Aidha, amewahimiza vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi, akieleza kuwa stadi hizo huwapa uwezo wa kujiajiri, kubuni teknolojia na kuanzisha biashara badala ya kusubiri ajira rasmi.Amesema iwapo vijana wengi wataamua kujifunza stadi za ufundi na kuzitumia kwa ubunifu, changamoto ya ajira itapungua huku sekta za uzalishaji na uchakataji wa mazao zikiendelea kukua na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.


