UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefanikisha kuwafikishia huduma za mawasiliano wananchi wapatao milioni 8.5 kupitia ujenzi wa minara 758 iliyotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 126, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma hizo nchini.

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Novemba 03,2026, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

1003617346 UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Amesema tangu mwaka 2012, mfuko huo umeingia mikataba ya ujenzi wa minara 2,324 katika awamu 21, ambapo minara 2,199 imekamilika, huku ukiendelea na mradi mwingine wa ujenzi wa minara 287 kwa gharama ya Sh bilioni 29.

Richard amesema miradi hiyo inalenga kupanua upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ambayo watoa huduma hawana hamasa ya kibiashara ya kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Katika hatua nyingine, amesema UCSAF inaendelea na juhudi za kuongeza upatikanaji wa intaneti katika maeneo ya wazi kupitia huduma za Public WiFi, lakini changamoto kubwa ni gharama za uendeshaji na kupata mfumo endelevu wa kugharamia huduma hizo baada ya miundombinu kukamilika.

1003616015 UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2024/25, huku katika mwaka wa fedha 2025/26 mfuko ukiwa na mpango wa kufikisha huduma hiyo katika maeneo 60 Tanzania Bara na Zanzibar.

Amefafanua kuwa UCSAF inatafuta mfumo utakaowawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi na gharama nafuu, ikiwamo utaratibu wa kuwapatia watumiaji muda wa awali wa intaneti bila malipo kabla ya kuendelea na huduma kwa malipo.

Richard amesema mfumo huo unalenga kuongeza matumizi ya teknolojia na kuwapa wananchi fursa ya kupata taarifa, kufanya shughuli mbalimbali za kidijitali na kuwasiliana kwa urahisi.

1003616051 UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Alisema pia zaidi ya maeneo 15 yamehusishwa katika mradi wa redio za jamii unaojumuisha ujenzi wa minara na studio kwa gharama ya Sh bilioni sita, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

Katika sekta ya elimu, Richard amesema zaidi ya shule 1,167 zimefaidika na mradi wa usambazaji wa vifaa vya TEHAMA kwa gharama ya takribani Sh bilioni 17.7, huku shule 22 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu zikipatiwa vifaa vinavyowawezesha kupata elimu ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Sabatho Kosuli, amesema UCSAF ni taasisi ya kimkakati katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii kwa kuwa huduma za mawasiliano zinafungua fursa za ajira, biashara na uchumi wa kidijitali.

1003616009 UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 unahitaji uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia, hivyo akawataka waandishi wa habari kuelimisha wananchi kuhusu miradi inayotekelezwa na fursa zinazotokana na upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.

1003616121-1024x683 UCSAF yafikisha Mawasiliano kwa Wananchi Milioni 8.5

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *