
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi ambapo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2025, pato halisi la Taifa limekua kwa asilimia 6.0 ikilinganishwa na asilimia 5.5 kipindi kama hicho mwaka 2024.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo April 01,2026, Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2026/2027.
Dkt. Mwigulu amesema “Ukuaji huo umechangiwa na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ikiwamo nishati, mawasiliano, usafiri na usafirishaji, huduma za kijami na kuimarıka kwa shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi”
“Nchi yetu imeendelea kuwa na utulivu wa bei uliotokana na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, kuimarika kwa bei ya mafuta na bidhaa katika soko la dunia na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani, utulivu huo ulichangia kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya bidhaa na huduma.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2025, wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.5. Kiwango hicho kipo ndani ya lengo la nchi la asilimia 3.0 hadi 5.0.
“Mfumuko wa bei kwa Januari, 2026 ulikuwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2025, kiwango hicho kipo ndani ya lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki la kutozidi asilimia 8.0 na lengo la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la asilimia 3.0 hadi 7.0”
“Serikali itaendelea kufuatilia hali ya kisiasa na kiuchumi duniani na kuchukua hatua stahiki ili kuwa na utulivu wa mwenendo wa bei za bidhaa”






