TCDC Kuendelea Kuboresha Mifumo ya Kidigitali Katika SACCOS

IMG-20261014-WA0006-1024x682 TCDC Kuendelea Kuboresha Mifumo ya Kidigitali Katika SACCOS

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), imesema inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali katika vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza matumizi ya makaratasi na kuwavutia vijana wengi zaidi kujiunga na vyama hivyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika anayeshughulikia Udhibiti kutoka TCDC, Collins Nyakunga wakati wa Kongamano ya 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA) linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026 huku zaidi ya watu 1200 wakishiriki.

Amesema matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za ushirika na kuendana na mahitaji ya vijana ambao kwa sasa wanapendelea kutumia simu na mifumo ya kielektroniki kufanya shughuli mbalimbali

Nyakunga amesema Serikali imewezesha kuanzishwa kwa Mifumo wa Usimamizi wa Kielektroniki wa Vyama vya Ushirika (MUVU), unaorahisisha usajili wa vyama na ukusanyaji wa taarifa muhimu za uendeshaji wake.

Amesema kupitia mfumo huo, TCDC inaweza kupata taarifa za vyama vya ushirika kwa wakati, ikiwemo ripoti za utendaji zinazowasilishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo.

“Serikali ya Awamu ya Sita imetoa msaada mkubwa katika kuendeleza sekta ya ushirika. Tumeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao unarahisisha usajili wa vyama vya ushirika na upatikanaji wa taarifa zake, hivyo kufanya usimamizi kuwa rahisi zaidi,” amesema Nyakunga.

Ameongeza kuwa TCDC imetoa maelekezo kwa kila SACCOS kuwa na mfumo wa TEHAMA utakaosaidia shughuli za kiutawala, uhasibu na utoaji wa huduma kwa wanachama, ikiwemo kutumia programu za simu kuomba mikopo na kupata huduma nyingine.

IMG-20261014-WA0007-1024x682 TCDC Kuendelea Kuboresha Mifumo ya Kidigitali Katika SACCOS

Amesema mifumo hiyo inapaswa kuunganishwa na mfumo mkuu wa TCDC ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa zinazohitajika kwa ajili ya usimamizi na udhibiti wa vyama hivyo.

Nyakunga amesema hatua hiyo pia inalenga kupunguza urasimu na muda unaotumika katika kujiunga na SACCOS, huku matumizi ya mifumo isiyotegemea makaratasi yakitarajiwa kurahisisha huduma na kuongeza mvuto wa vyama hivyo kwa vijana.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika bodi na nafasi za kiutendaji za SACCOS ili kuleta mawazo mapya, kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kuboresha huduma zinazotolewa.

Amesema sekta ya ushirika inahitaji kufanya utafiti wa mara kwa mara ili kutambua mahitaji ya wananchi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi na kiteknolojia.

Akizungumzia faida za kujiunga na SACCOS, Nyakunga amesema wanachama wana nafasi ya kunufaika kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupata mikopo, kuweka akiba na kupokea gawio pale chama kinapopata faida na kutangaza gawio kwa mujibu wa taratibu zake.

Ameeleza kuwa tofauti na kuwa wanufaika wa huduma, wanachama pia ni wamiliki na wawekezaji katika vyama vyao, hivyo wana nafasi ya kushiriki katika maamuzi kuhusu uendeshaji na huduma zinazotolewa.

Katika hatua nyingine, Nyakunga amesema kongamano la ushirika wa akiba na mikopo barani Afrika ni fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora na kujadili namna ya kuimarisha maendeleo ya sekta ya ushirika.

Amesema kongamano hilo pia lina mchango katika kuitangaza Tanzania kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali, ambao wanapata fursa ya kujifunza kuhusu utamaduni, vivutio vya utalii na fursa za kiuchumi zilizopo nchini.

IMG-20261014-WA0004-1024x683 TCDC Kuendelea Kuboresha Mifumo ya Kidigitali Katika SACCOS
IMG-20261014-WA0005-1024x683 TCDC Kuendelea Kuboresha Mifumo ya Kidigitali Katika SACCOS

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *