TCB yazidi kupaa, makusanyo ya uwekezaji yaongezeka mara tatu

-Yakusanya bil.140.24/- ikiwa ni mara tatu ya lengo la bil. 50/-

-Mazingira ya uwekezaji yazidi kuwa rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imetangaza mafanikio ya kuweka rekodi mpya katika masoko ya mitaji nchini baada ya kupokea uwekezwaji wa kiwango cha juu cha asilimia 281 na kukusanya Sh. bilioni 140.24 na kupitisha lengo la awali la Sh. bilioni 50.

Hatifungani ya Stawi iliidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Septemba 11, 2025 na kutolewa chini ya awamu ya kwanza ya Waraka wa Matarajio wa Programu ya Miaka Mitano wenye thamani ya Sh. bilioni 150 za Kitanzania.

Hatifungani hiyo ilitoa riba shindani ya asilimia 13.5, inayolipwa kila baada ya robo mwaka kwa kipindi cha miaka mitano, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Sh. 500,000 na hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa fursa za uwekezaji zenye mvuto mkubwa na zinazowafikia Watanzania wengi.

Uuzaji wa Awali kwa Umma (IPO), uliofunguliwa Septemba 17, 2025 na kufungwa Oktoba 17, 2025, ulipokea mwitikio mkubwa kutoka kwa wawekezaji nchini kote.

Akizungumza katika hafla hiyo jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo, ameeleza kuwa matokeo hayo ni hatua muhimu ya kihistoria kwa benki na kwa masoko ya mitaji nchini kwa ujumla.

“Ukusanyaji wa Sh. bilioni 140.24, karibu mara tatu ya lengo letu la awali unaonesha imani kubwa ambayo Watanzania wameiweka katika dira ya TCB pamoja na dhamira yetu ya kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi,” alisema Mihayo. “Kinachofanya hatua hii kuwa ya kipekee zaidi ni ushiriki mkubwa na wa kiwango cha juu kutoka kwa wawekezaji wadogo na wa kati yaani Watanzania wa kawaida waliotumia fursa hii kuwekeza katika bidhaa salama na yenye tija.”

Tofauti na hatifungani nyingine ambazo mara nyingi hutawaliwa na uwekezaji wakubwa wa mashirika na kampuni, Hatifungani ya Stawi ilivutia ushiriki mkubwa kutoka kwa wawekezaji binafsi. Hii ni ishara muhimu ya kuimarika kwa ujumuishi wa kifedha na ongezeko la ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji.

Kwa idhini ya CMSA, TCB imethibitisha kuwa itapokea kiasi chote cha Sh. bilioni 140.2 kilichowekezwa, na kwamba maombi yote halali yatapata mgao wa asilimia 100.

Mihayo aliwashukuru wadau muhimu waliochangia mafanikio ya uwekezaji huu, wakiwamo, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), iTrust Finance Limited – Mshauri Mkuu wa Muamala na Dalali Mdhamini, Endoxa Law – Washauri wa Kisheria na Auditax International – Wakaguzi

“Kwa wawekezaji wote wakiwamo taasisi, watu binafsi, na hasa wale waliowekeza kwa mara ya kwanza, tunatoa shukrani zetu za dhati. Imani yenu ndiyo inayotupa nguvu ya kuendelea,” ameongeza.

“TCB itaendelea kubuni bidhaa bunifu za kifedha zinazowawezesha watu, kuimarisha jamii, na kuchangia mabadiliko ya kiuchumi ya Taifa.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema, “Kupitia Hatifungani ya Stawi, TCB imefungua milango kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki katika masoko ya mitaji, kukuza uchumi wao, na kuchangia katika kuunda mustakabali wa uchumi wetu. Imani iliyooneshwa na wananchi si uthibitisho tu wa ubora wa bidhaa hii ya kifedha, bali pia ni imani kwa TCB kama taasisi imara, yenye maono na inayojitolea kwa maendeleo ya taifa.”

Khamis aliongeza kuwa, “Serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Fedha, itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha kustawi. Tumejipanga kupanua njia za upatikanaji wa fedha, kukuza huduma za mikopo nafuu, na kuhakikisha kuwa biashara ndogo na za kati (SMEs) zinapata mitaji inayohitajika kukuza shughuli zao. Kwa kufanya hivyo, tunalenga kukuza ujumuishi wa kifedha, ujasiriamali na uwezeshaji kiuchumi, nguzo muhimu za ajenda yetu ya maendeleo ya taifa.”

Mafanikio ya Hatifungani ya Stawi yanaonesha mkakati wa TCB wa kuimarisha mtaji wake, kuendelea kuzisaidia biashara ndogo na za kati, na kuwekeza katika ubunifu wa kidijitali kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma nchini kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *