
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUMI ya Tanzania Breweries PLC (TBL) imeadhimisha Siku ya Maji Duniani kwa vitendo kwa kuongoza zoezi la usafi lililowakutanisha viongozi wa jiji, zaidi ya wafanyakazi 100 pamoja na wadau wa jamii katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo lililenga kusafisha na kurejesha njia ya kupitisha maji taka (effluent discharge channel), eneo muhimu katika kulinda mifumo ya maji na afya ya mazingira kwa ujumla.
Shughuli hiyo ilifanyika kwa ushirikiano na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma, pamoja na viongozi wa Manispaa ya Ilala na madiwani wa maeneo husika.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TBL, Neema Temba, amesema kampuni hiyo inaweka mkazo katika vitendo endelevu vya kulinda rasilimali maji.
“Maji ni mhimili wa biashara yetu na maisha ya jamii. Tunawajibika kuyatunza ndani ya shughuli zetu na katika mazingira tunayofanyia kazi. Ushirikiano huu unaonesha namna tunavyoweza kutoa suluhisho la kudumu kwa usalama wa maji,” amesema Temba.
Ameongeza kuwa, juhudi za kulinda maji zinahitaji mshikamano wa wadau mbalimbali na utekelezaji wa vitendo vinavyoleta matokeo halisi kwa jamii.
Kwa upande wake, Meya Juma, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kulinda mazingira ya mijini.
“Usafi wa jiji na ulinzi wa mifumo ya maji ni jukumu la kila mmoja wetu. Ushirikiano huu unasaidia kuboresha afya ya jamii na kujenga jiji endelevu,” amesema.
Mbali na zoezi hilo, TBL inaendelea kuwekeza katika miradi ya muda mrefu ya uhifadhi wa maji kwa kushirikiana na WWF Tanzania. Miradi hiyo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji safi katika maeneo ya Kibaha kupitia miundombinu inayotumia nishati ya jua, pamoja na kulinda vyanzo vya maji na mifumo ya ikolojia.
Aidha, ushirikiano huo unahusisha juhudi za kulinda na kurejesha vyanzo muhimu vya maji kama mito ya Msimbazi, Kizinga na Ruvu, ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa maji wa muda mrefu katika jiji la Dar es Salaam.
Ingawa zoezi la usafi lilikuwa la eneo maalum, limeakisi dhamira pana ya kampuni hiyo katika usimamizi bora wa rasilimali maji na umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za mazingira.

