Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

1003386126-1024x804 Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 10 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Masuala ya Usafiri wa Majini kwa Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA), utakaowakutanisha takribani mawaziri 26 wanaoshughulikia masuala ya uchukuzi na lojistiki kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuimarisha biashara na usafirishaji wa majini barani Afrika.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba utakua na ajenda mbalimbali zinazolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama, kupanua usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli na kuongeza ushiriki wa Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.

1003386124-1024x682 Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, aliyetoa taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, alisema mkutano huo utajadili masuala muhimu ya maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini kwa nchi wanachama wa MOESNA.

Anasema shirika hilo linajumuisha nchi zenye ukanda wa bahari na zile zisizo na mwambao wa bahari, ambazo zinahitaji ushirikiano katika kuimarisha mifumo ya usafirishaji na kuwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Anasema mawaziri watakaoshiriki mkutano huo wanatoka nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Burundi, Botswana, Malawi, Angola, Comoro, Djibouti, Misri, Eritrea, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Somalia, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Sudan na Zimbabwe.

1003386123-1024x682 Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

Kihenzile anasema moja ya ajenda muhimu za mkutano huo ni kujadili namna ya kukuza biashara kwa kupanua wigo wa usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli kati ya bandari za Afrika katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Anasema hatua hiyo inalenga kujenga mazingira wezeshi yatakayoongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika usafirishaji wa majini na kuhamasisha uanzishwaji wa mashirika ya meli ya Afrika yatakayoweza kushindana na mashirika makubwa ya meli duniani.

anasema ushiriki wa mashirika ya meli kutoka Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa unatarajiwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya usafirishaji wa majini, kufungua fursa za ajira kwa vijana na mabaharia na kuimarisha biashara baina ya nchi wanachama wa MOESNA.

Mkutano huo pia unafanyika katika kipindi ambacho nchi za Afrika zinaendelea kutekeleza Agenda 2063 yenye kaulimbiu ya ‘Afrika Tuitakayo’ na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), unaolenga kuondoa vikwazo vya kibiashara, kujenga soko kubwa la bidhaa, kuongeza biashara baina ya nchi za Afrika na kukuza viwanda.

1003386125-1-1024x682 Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

Katika maelezo yake, Kihenzile anasisitiza umuhimu wa usafiri wa majini katika uchumi wa dunia, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya Afrika husafirishwa kwa njia ya bahari, huku zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo ikipitia njia hiyo.

Anasema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha bandari, huduma za meli na mifumo ya usafirishaji inayounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko ili kuongeza uwezo wa Afrika kushindana katika biashara ya kimataifa.

Anasema Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi na maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, jambo linaloiweka katika nafasi muhimu ya kuwezesha biashara kati ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini na masoko ya dunia.

Kupitia mkutano huo, nchi wanachama wa MOESNA zitapata fursa ya kujadili mikakati ya pamoja ya kuimarisha usafiri wa majini, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria na kupanua fursa za biashara na uwekezaji katika sekta hiyo.

1003386127-1024x860 Tanzania mwenyeji Mkutano wa Mawaziri 26 wa MOESNA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *