-Dkt.Homera ataka kasi utekelezaji

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Novemba 16, 2026, limewasilisha kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, mpango wa kufikisha uwezo wa uzalishaji umeme hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya viongozi wakuu wa nchi pamoja na Mpango wa Taifa wa Nishati wa 2025-2030.
Mpango huo unahusisha miradi inayotekelezwa na ile iliyopo katika hatua mbalimbali za maandalizi ambayo kwa ujumla inatarajiwa kuongeza jumla ya Megawati 3,856.5 kwenye gridi ya taifa.
Kikao cha kuwasilisha mpango huo kimefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa miradi iliyowasilishwa ni Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 49.5, ambao umefikia asilimia 33 ya utekelezaji.
Mingine ni Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa Megawati 100 pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua wa Zuzu mkoani Dodoma wenye uwezo wa Megawati 130, ambapo maandalizi ya awali yanaendelea.
Mradi mwingine uliowasilishwa ni wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma mkoani Njombe, wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,000 na unaokadiriwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 2.5. Mradi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa itakayoongeza uwezo wa uzalishaji umeme nchini na kuchangia uzalishaji kwa kipindi cha zaidi ya miaka 56.
Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa inahusisha matumizi ya nishati ya upepo, gesi asilia na jua katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Makambako (MW 100), Singida (MW 200), Mkuranga (MW 177) na Dodoma (MW 100). Miradi hiyo ipo katika hatua za majadiliano ya mikataba ya ununuzi wa umeme na maandalizi ya utekelezaji.
Akizungumza baada ya kupokea mpango huo, Dkt. Homera ameitaka TANESCO kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuhakikisha kuwa majadiliano ya miradi ambayo bado haijaanza kutekelezwa yanakamilika ifikapo Februari 2027 ili kuwezesha kuanza kwa utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa miradi hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuwezesha uwekezaji katika viwanda, kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi.







